DIWANI MSTAAFU BENARD MWAKYEMBE ATIA NIA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA TEMEKE.
Diwani mstaafu wa Kata ya Mtoni, Benard Mwakyembe, ametangaza rasmi nia ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Temeke kupitia chama cha Mapinduzi (CCM),akiahidi kuleta mageuzi chanya katika sekta ya miundombinu, ajira kwa vijana, elimu na usimamizi wa fedha za maendeleo ya jamii.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu ya kugombea, Mwakyembe amesema kuwa endapo atapata ridhaa ya wananchi wa Temeke, atahakikisha kuwa miradi ya miundombinu hasa barabara, mifereji ya maji na huduma za kijamii inaboreshwa kwa kiwango kikubwa ili kurahisisha maisha ya wakazi wa jimbo hilo.
“Jimbo letu lina changamoto nyingi, lakini kubwa zaidi ni ukosefu wa miundombinu bora, ajira kwa vijana, na usimamizi hafifu wa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri yanayopaswa kwenda kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Nitahakikisha fedha hizi zinawafikia walengwa kwa wakati na kwa uwazi,” alisema Mwakyembe.
Aidha, ameweka mkazo katika suala la elimu, akiahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha shule za kata zinajengwa na kuboreshwa ili watoto wote wapate elimu katika mazingira rafiki.
Benard Mwakyembe ni miongoni mwa viongozi waliowahi kuhudumu kwa mafanikio makubwa kama Diwani wa Kata ya Mtoni. Anajivunia rekodi ya utendaji thabiti uliogusa maisha ya wananchi, na anaamini kuwa uzoefu huo unampa msingi imara wa kuliongoza Jimbo la Temeke akiwa Mbunge.



Comments
Post a Comment