MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.
Na Fidea Masunga,Dar es Salaam.
Wazazi na walezi nchini wametakiwa kuhakikisha wanawalea watoto katika misingi ya maadili, nidhamu na hofu ya Mungu ili kujenga kizazi chenye kuzingatia elimu, kuishi maisha ya wema na kuwa viongozi bora wa kesho.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na mdau wa elimu Ramadhan Balle, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya nane ya Shule ya Awali na Msingi Sai yaliyofanyika Chanika Kidugalo Dar es salaam.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balle alisema malezi bora ya watoto hayapaswi kuishia nyumbani pekee, bali yazingatie misingi ya kiroho kupitia maandiko ya dini kama Biblia na Qur’ani, kwani ndiyo msingi wa kujenga jamii yenye hofu ya Mungu na kuondokana na vitendo vya ukatili na maovu.
“Watoto wakilelewa katika msingi wa dini, wanakua na mwelekeo bora, wanajengeka kiakili na kiroho na hivyo kuepuka kujiingiza katika tabia hatarishi. Hili ni jukumu lenu wazazi na walezi,” alisema Balle.
Aidha, aliwataka wazazi kuwekeza zaidi katika malezi ya kimwili, kiakili na kimaadili badala ya kuachia jukumu hilo walimu pekee.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Samwel Mandoo, alisema taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha inaendelea kutoa elimu bora sambamba na malezi ya maadili, nidhamu na usalama wa wanafunzi.
“Shule yetu haijajikita tu kwenye ufaulu wa kitaaluma, bali pia kwenye kujenga nidhamu na misingi ya maadili kwa kila mtoto. Tunaamini elimu bila malezi bora haikamiliki,” alisema Mandoo.
Mariam Mdumi na Frank Yusuf ni baadhi ya wahitimu wa darasa la saba katika shule hiyo walipata nafasi ya kueleza furaha yao, wakisema malezi na elimu waliyoipata yamewajenga kielimu, kitabia na kimaadili.
“Tumejifunza nidhamu, heshima na kumcha Mungu pamoja na masomo yetu ya kila siku. Tunashukuru walimu wetu na wazazi kwa kushirikiana kutufanya tuwe tulivyo leo,” alisema mmoja wa wahitimu.
Mahafali hayo yalihudhuriwa pia na wazazi, walezi na wadau wa elimu waliohudhuria kwa wingi na kushuhudia burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya awali hadi darasa la saba.
Nao baadhi ya wazazi walipongeza juhudi za walimu na uongozi wa shule hiyo kwa kuendelea kusimamia elimu na malezi bora, wakiahidi kushirikiana nao katika kuhakikisha watoto wanakua kwenye msingi wa nidhamu na hofu ya Mungu.
Katika mahafali hayo, jumla ya wanafunzi 36 wa darasa la saba wamehitimu elimu ya msingi, wakiwamo wasichana 22 na wavulana 14.
Shule hiyo pia imeendelea kujivunia ufaulu wa asilimia 100 kwa wanafunzi wake wa darasa la saba, jambo ambalo limeifanya kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vizuri katika eneo la Chanika na Dar es Salaam kwa ujumla.





BravooooooooooooMzee NDEREKA mungu akubariki sana tena sana Kwa kuhakikisha msingi Bora ya Elimu, nidhamu , maadili na hogu ya mungu vina imarika ipasavyo
ReplyDelete