SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI: POLISI WANAMAJI WATEMBELEA WAGONJWA NA KUTOA MSAADA.
Jeshi la Polisi Kikosi cha Wanamaji jijini Dar es Salaam limefanya zoezi la kutoa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Kilwa Road, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia na Watoto.
Zoezi hilo lililofanyika jijini Dar es salaam limelenga kuongeza faraja kwa wagonjwa hasa wale wanaokabiliwa na changamoto za kifedha, na kuonyesha dhamira ya Jeshi la Polisi katika kuchangia ustawi wa jamii ambapo mahitaji yaliyotolewa yanatarajiwa kusaidia wagonjwa kupata huduma wanazokosa kwa wakati kutokana na ukosefu wa uwezo wa kifedha.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Afya, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Lucas Mkondya, alikipongeza Kikosi cha Wanamaji kwa kujitoa kwao, akieleza kuwa hatua hiyo imeonyesha kuguswa kwao na changamoto wanazopitia wagonjwa wengi.
Aidha, Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji jijini Dar es Salaam, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Twahiri Lyimo, alishukuru uongozi wa Hospitali ya Kilwa Road kwa ushirikiano wao katika kufanikisha tukio hilo, akiamini kuwa msaada uliotolewa utawasaidia wagonjwa kwa kiwango kikubwa.
Wagonjwa waliopokea mahitaji hayo wamepongeza hatua hiyo ya Jeshi la Polisi, wakisema imetoa matumaini na faraja katika kipindi kigumu cha matibabu.
Zoezi hilo limeendelea kuonyesha mshikamano kati ya vyombo vya ulinzi na jamii, sambamba na kuunga mkono kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia na watoto nchini.

Comments
Post a Comment