𝐖𝐀𝐓𝐀𝐋𝐈𝐈 𝐖𝐀𝐎𝐍𝐆𝐄𝐙𝐄𝐊𝐀 𝐊𝐖𝐀 𝐀𝐒𝐈𝐋𝐈𝐌𝐈𝐀 𝟐𝟎 𝐊𝐀𝐓𝐈𝐊𝐀 𝐌𝐈𝐒𝐈𝐓𝐔 𝐘𝐀 𝐓𝐅𝐒.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Idadi ya watalii wanaotembelea vivutio vya utalii ikolojia vinavyosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imeongezeka kwa asilimia 20 katika kipindi cha mwaka mmoja, hatua inayoonyesha kuimarika kwa sekta ya utalii wa mazingira nchini.


Akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2026/2027 bungeni Dodoma Mei 15, 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji alisema watalii 329,753 walitembelea vituo vya utalii ikolojia hadi Aprili 2026 ikilinganishwa na watalii 275,723 waliorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.


Alisema ongezeko hilo limechangia mapato ya utalii kufikia Sh bilioni 3.09 kutoka Sh bilioni 2.16 mwaka uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 43.


Kwa mujibu wa Waziri huyo, TFS imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii kwa kujenga malango sita ya utalii katika maeneo mbalimbali yakiwemo Meru, Vikindu, Mlima Rungwe na Ziwa Duluti.


Aidha, kilomita 287.14 za njia za watembea kwa miguu na barabara za ndani ya misitu zimekarabatiwa pamoja na kambi nane za watalii ili kuongeza ubora wa huduma kwa wageni wanaotembelea maeneo hayo.


Katika juhudi za kuhamasisha utalii wa mazingira, TFS pia imeendesha matamasha mbalimbali ya utalii na michezo ya mazingira yakiwemo “Tukutane Mt. Rungwe Season II”, “Lake Ngosi”, “Meru Adventure Race” na “Kalambo Waterfalls Utalii Festival”, yaliyovutia maelfu ya washiriki na watalii.


Kwa mwaka 2026/2027, TFS imepanga kuendelea kuimarisha miundombinu ya utalii ikolojia kuelekea matukio makubwa ya kimataifa yakiwemo AFCON na Miss World.


𝐓𝐀𝐊𝐖𝐈𝐌𝐔 𝐙𝐀 𝐔𝐓𝐀𝐋𝐈𝐈

• Watalii 2025/26: 329,753

• Watalii 2024/25: 275,723

• Ongezeko la watalii: 20%

• Mapato 2025/26: Sh bilioni 3.09

• Ongezeko la mapato: 43%




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.