KICHWA CHA JAMES TEMBA CHAPATIKANA KITUNDA, MGANGA WA KIENYEJI AKAMATWA.
Kichwa cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), James Temba, kimepatikana katika eneo la Kitunda Kibeberu, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, baada ya juhudi za uchunguzi wa Jeshi la Polisi kuendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari Mei 13, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kichwa hicho kilikutwa kikiwa kimefukiwa ardhini.
Muliro amesema jumla ya watu watano wanashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, akiwemo mganga wa kienyeji aliyefahamika kwa jina la Said Ally maarufu “Side”, mwenye umri wa miaka 31.
“Sehemu ya kichwa hiki kimekutwa kimefukiwa ardhini na waliotekeleza uhalifu ule. Jumla ya watuhumiwa watano wanashikiliwa,” amesema.
Ameongeza kuwa taratibu za kisheria zinaendelea kukamilishwa ili kuruhusu hatua nyingine za uchunguzi na sheria dhidi ya watuhumiwa hao.
Kwa upande wake, baba mzazi wa marehemu, Rogers Temba, amesema kwa njia ya simu kuwa alipata taarifa za awali kuhusu kupatikana kwa kichwa hicho katika eneo la Kitunda Kibeberu huku polisi wakiendelea na uchunguzi zaidi.
Mwili wa James Temba ulizikwa Mei 7, 2026 katika makaburi ya familia yaliyopo Kijiji cha Mande, Kata ya Old Moshi Magharibi, Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, ukiwa hauna kichwa.

Comments
Post a Comment