MKURUGENZI WA RASILIMALI WATU TANESCO AWAHAKIKISHIA USHIRIKIANO MAAFISA HUDUMA KWA WATEJA KUBORESHA UTENDAJI.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala TANESCO, Bi. Beatrice Kimoleta, amewahakikishia Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja ushirikiano katika kufanikisha upatikanaji wa nyenzo muhimu zitakazowawezesha kuhudumia wateja kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu.
Ametoa kauli hiyo Mei 22, 2026 alipokuwa akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa maafisa hao uliofanyika kwa siku tano kuanzia Mei 18, 2026 jijini Dodoma, mkutano ambao hufanyika kila mwaka kwa lengo la kufanya tathmini ya kuboresha utendaji kazi wa kurugenzi ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.
“Kwa uongozi wa Shirika, kipaumbele chetu ni kuhakikisha watumishi wanaohudumia wateja moja kwa moja wanakuwa katika mazingira mazuri ya kazi ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi. Tunawahakikishia kuwapatia nyenzo muhimu ili muendelee kutoa huduma bora kwa wateja,” ameeleza , Bi. Kimoleta .
Ameeleza kuwa, Uongozi wa Shirika unatambua kazi kubwa inayofanywa na Maafisa hao katika kulipa Shirika sifa njema na utendaji unaojenga imani ya Serikali na Shirika kwa wananchi kupitia utoaji wa huduma bora na yenye ufanisi kwa wateja.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwahudumia wateja kwa kujituma. Mchango wenu unajenga taswira chanya ya Serikali na Shirika kwa wananchi. Endeleeni kudumisha uadilifu na weledi katika utendaji kazi wenu.” amebainisha.
Pamoja na hayo, amesisitiza umuhimu wa umakini na uwajibikaji katika kuyafanyia kazi mafunzo ya kujengeana uwezo yaliyotolewa katika mkutano huo muhimu, ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha utendaji bora wenye kuleta matokeo chanya.
“Kundi hili ni muhimu sana katika kulinda taswira ya Shirika. Ninaamini mafunzo mliyopata kwenye mkutano huu yatakuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma. Nawahimiza ushirikiano katika kujengana kiutendaji .” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja TANESCO, Bi. Irene Gowelle, ameushukuru uongozi wa Shirika kwa kuwezesha kufanyika kwa mkutano huo, akisema umetoa fursa kwa maafisa kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wateja. Aidha, amepongeza kujituma na weledi wa maafisa hao katika utekelezaji wa majukumu yao.
“ Najivunia kuongoza kundi hili la watoa huduma kwa wateja kutokana na ufanisi wao mkubwa, hasa wakati wa changamoto, kwa kujitolea kufanya kazi kwa ziada na kuhudumia wateja kwa weledi wa hali ya juu,” ameeleza, Bi. Gowelle.
Mwenyekiti wa Mkutano huo , Bw. Amon Bidebuye akizungumza kwa niaba ya Maafisa wenzie ameahidi utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Viongozi katika kuleta mapinduzi ya utoaji wa huduma kwa wateja kuendana na ukuaji wa teknolojia.



Comments
Post a Comment