MWENGE WA UHURU WAZINDUA MRADI WA UMEME WA BILIONI 4.17 NYASA.
Mwenge wa Uhuru 2026 umezindua mradi wa kusambaza umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Kitongoji cha Ndecha Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.17, hatua inayotarajiwa kuongeza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa eneo hilo.
Akizindua mradi huo Mei 16, 2026, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, alisema Serikali imeendelea kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi wa vijijini kwa gharama nafuu ili kuboresha maisha yao.
Mwang’onda aliwahamasisha wananchi kujitokeza kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 pekee, akisema huduma hiyo sasa ipo karibu na wananchi tofauti na zamani ambapo gharama zilikuwa kubwa zaidi.
“Tunataka wananchi wachangamkie fursa hii ya umeme wa shilingi 27,000 ili kila nyumba iweze kupata huduma ya nishati na kuchochea maendeleo,” alisema.
Msimamizi wa Miradi ya REA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Hamisi Mrope, alisema mradi wa REDP2C katika Wilaya ya Nyasa ulianza Novemba 16, 2023 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2026.
Alisema mradi huo unahusisha vitongoji 30, mashine umba 30 pamoja na kuunganisha wateja 1,247 kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 4.17.
Katika Kitongoji cha Ndecha pekee, alisema kilomita 8.43 za njia ya umeme zimejengwa, mashine umba mbili zimefungwa na wateja 94 wanatarajiwa kuunganishiwa huduma hiyo kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 307.6.
Aidha, alisema miundombinu ya mradi imekamilika kwa asilimia 100 huku wananchi 56 tayari wakiwa wameunganishiwa umeme.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya MF Electrical Engineering Ltd chini ya usimamizi wa TANESCO.
Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Mhe. John Nchimbi, alisema miradi ya REA imewezesha vijiji vyote 84 vya wilaya hiyo kupata huduma ya umeme, jambo ambalo limeendelea kuchochea maendeleo kwa wananchi.
Naye Mhandisi Mussa David kutoka MF Electrical Engineering Ltd alisema tayari nyumba 56 zimewashiwa umeme katika Kitongoji cha Ndecha.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo wakisema itasaidia kuongeza shughuli za biashara na kuboresha maisha yao baada ya kuondokana na matumizi ya taa za vibatari na nishati zisizo salama.
Uzinduzi wa mradi huo umeenda sambamba na kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru 2026 inayosema, “Tanzania ni Yetu Sote, Tushikamane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo.”



Comments
Post a Comment