SERIKALI KUJENGA KIWANDA CHA SARUJI HANANG


Serikali imesema inaendelea kutafuta mwekezaji wa uhakika kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha saruji katika Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara, kutokana na kuwepo kwa malighafi za kutosha zinazohitajika katika uzalishaji wa saruji.


Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, Mei 11, 2026 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali namba 305 la Mbunge wa Hanang, Asia Halamga, lililouliza kuhusu mpango wa Serikali wa kuanzisha kiwanda hicho.


Naibu Waziri Londo amesema Serikali inatambua uwepo wa malighafi muhimu kwa ajili ya uzalishaji wa saruji katika Wilaya ya Hanang na tayari imeanza kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa mradi huo.


Ameeleza kuwa Serikali imetenga ekari 360 kwa ajili ya mradi huo, ambapo ekari 300 ni kwa ajili ya malighafi na ekari 60 zitajengwa kiwanda, huku mchakato wa kutafuta mwekezaji ukiendelea ili kuhakikisha mradi unatekelezwa na kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi wa eneo hilo.


Aidha, amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kuanzisha viwanda vya kimkakati kulingana na rasilimali zilizopo katika kila mkoa.


Ameongeza kuwa mbali na saruji, Hanang ina fursa nyingine za kiuchumi zikiwemo malighafi za uzalishaji wa chumvi pamoja na zao la ngano, ambazo Serikali inazifanyia maandalizi kwa ajili ya uwekezaji wa kuongeza thamani ili kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi.


Katika hatua nyingine, Londo amesema mkakati wa maendeleo ya viwanda hautaishia Hanang pekee, bali utaenea katika Wilaya ya Babati na maeneo mengine nchini kupitia uanzishwaji wa kanda maalum za uwekezaji, kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao, kukuza mauzo ya nje na kuinua uchumi wa wananchi kwa ujumla.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.