TLS YATAKA CHOMBO HURU KUCHUNGUZA VURUGU ZA UCHAGUZI MKUU 2025.
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetoa wito wa kuundwa kwa chombo huru, shirikishi na cha kuaminika kwa ajili ya kuchunguza matukio ya vurugu yaliyotokea kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi amesema mapendekezo hayo yametolewa kufuatia tathmini ya chama hicho kuhusu ripoti ya tume ya Jaji Chande iliyohusu matukio ya Oktoba 29, 2025.
Amesema TLS inaamini kuwa taifa linahitaji kuponya majeraha ya kisiasa na kijamii kupitia misingi ya haki, ukweli, uwajibikaji na maridhiano ya kweli ili kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za dola na mfumo wa utoaji haki.
Katika mapendekezo yake, TLS imependekeza kuundwa kwa chombo huru na shirikishi kitakachofanya uchunguzi wa kina kuhusu madai ya vurugu, ukiukwaji wa haki za binadamu na vitendo vya ukatili vilivyoripotiwa kujitokeza katika kipindi cha uchaguzi mkuu.
Aidha, chama hicho kimeitaka serikali kukiri makosa yaliyojitokeza wakati wa matukio hayo na kuhakikisha wahusika wote wa ukiukwaji wa haki wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
TLS pia imesisitiza kuwa mchakato wa maridhiano ya kitaifa hauwezi kuwa na tija bila kuwepo kwa ukweli, uwazi na uwajibikaji kwa pande zote zinazohusika.
Sambamba na hilo, chama hicho kimependekeza waathirika wa vifo, majeruhi na madhara mengine yaliyotokana na matukio hayo kufidiwa ili kusaidia kurejesha haki na faraja kwa waathirika pamoja na familia zao.
Kwa upande mwingine, TLS imesema ipo tayari kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali wa haki na utawala bora katika kutafuta suluhisho la kudumu kwa masuala hayo kwa maslahi ya taifa.
Akizungumzia mwenendo wa kesi ya Tundu Lissu, Wakili Mwabukusi ameieleza wasiwasi ya TLS kuhusu shauri hilo kuchukua muda mrefu bila kutolewa uamuzi, akisisitiza umuhimu wa haki kutendeka kwa wakati kwa mujibu wa sheria na Katiba.


Comments
Post a Comment