TMA NA BRAC MAENDELEO TANZANIA WAJADILI MIKAKATI YA KUIMARISHA USAMBAZAJI NA MATUMIZI YA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.
Dodoma
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na BRAC Maendeleo Tanzania wamejadili mikakati ya kuimarisha usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa nchini, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Majadiliano hayo yalifanyika Mei 15, 2026 katika Makao Makuu ya TMA jijini Dodoma yakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Chang’a alisema TMA inaendelea kuthamini ushirikiano na wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za hali ya hewa na kuhakikisha taarifa zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.
Alisema kikao hicho kimefungua fursa kwa taasisi hizo mbili kujadiliana maeneo ya ushirikiano katika utoaji wa huduma za hali ya hewa, tahadhari za mapema pamoja na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, alisema TMA ipo katika mageuzi ya kidigitali yanayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya kisasa ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa taarifa kwa jamii.
Dkt. Chang’a pia alieleza dhamira ya TMA kuendelea kuimarisha ushawishi wa Tanzania katika masuala ya hali ya hewa barani Afrika na katika nchi zinazoendelea, huku akiishukuru BRAC Maendeleo Tanzania kwa mchango wake katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi ya taarifa za hali ya hewa.
Vilevile, alihamasisha ushiriki wa wadau mbalimbali katika Mkutano wa Nne wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuhusu miongozo ya Utabiri wa Hali ya Hewa (Operational Climate Prediction-OCP4), unaotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Juni 29 hadi Julai 3, 2026.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Programu ya Hali ya Hewa ya Kimataifa wa BRAC Maendeleo Tanzania, Degefu Getachew Kelbiso, alieleza kuhusu utekelezaji wa mpango wa “BigBet” unaolenga kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kupitia huduma za taarifa za hali ya hewa, kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi pamoja na uimarishaji wa maisha ya jamii.
Alisema mpango huo unatekelezwa katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano na TMA katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia shughuli za kijamii na kiuchumi.



Comments
Post a Comment