Wafanyakazi waliopoteza ajira kulipwa mafao ndani ya siku 90.
Na OWM (KAM) - Dodoma
Serikali imetangaza maboresho ya kanuni za ulipaji wa mafao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ikiwemo fao la kukosa ajira, ili kuhakikisha wanachama wanapata haki zao kwa wakati na kuimarisha ustawi wao kiuchumi.
Hayo yameelezwa leo Mei 8, 2026 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Wilbard Munisi, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Ado Shaibu Ado.
Dkt. Munisi amesema Serikali imeboresha fao la kukosa ajira ambapo mfanyakazi aliyepoteza ajira ataweza kuchagua kulipwa mkupuo au kuendelea kupokea asilimia 33.3 ya mshahara wake kwa kipindi cha miezi sita, hatua inayolenga kumsaidia kuendelea kuwa na sifa za kupata pensheni baadaye.
Aidha, amesema Serikali imeweka utaratibu mpya wa mwaka 2025 unaomruhusu mfanyakazi aliyepoteza ajira kulipwa mafao yake kwa mkupuo ndani ya siku 90 tangu kupoteza ajira.
Amefafanua kuwa kwa sasa hakuna fao la kujitoa katika mifuko ya hifadhi ya jamii, bali kinachotambuliwa ni fao la kukosa ajira lililoboreshwa ili kuendana na hali ya soko la ajira na mahitaji ya wafanyakazi.
Serikali imesema maboresho hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii na kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa na usalama wa kipato wanapokumbwa na changamoto ya kupoteza ajira.


Comments
Post a Comment