WANAUME WATAKIWA KUWA MSTARI WA MBELE KATIKA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA.


Na Fidea Masunga, Dar es Salaam


Wanaume nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia unaowakumba wanawake na watoto, kuanzia ngazi ya familia hadi taifa, kwa kubadili mitazamo na mifumo dume inayochochea ukatili katika jamii.


Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam katika mdahalo wa kitaifa wa #SautiZetu ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), ukiwa na lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanaume katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mdahalo huo, Afisa Tarafa wa Wilaya ya Ubungo, Beatrice Mbawala, alisema mapambano dhidi ya ukatili hayawezi kuachiwa wanawake pekee, bali yanahitaji wanaume kusimama kama walinzi wa haki, usawa na utu katika jamii.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAMWA, Dk. Rose Reuben, alisema ukatili wa kijinsia si suala la wanawake pekee bali ni la haki za binadamu linalohitaji ushirikiano wa jamii nzima. Alisisitiza kuwa wanaume wanapaswa kubadili mitazamo na kushiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo hivyo.


Naye Agnes Mwafifi alisema mwanaume anatakiwa kuwa mlinzi kuanzia ngazi ya familia kwa kuhakikisha anasimamia maadili, usalama na ustawi wa wanajamii wake. Aliongeza kuwa nafasi ya mwanaume ndani ya familia ni msingi muhimu katika kuzuia ukatili wa kijinsia.


Hata hivyo, baadhi ya washiriki wa mdahalo huo walihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za wanawake na watoto, pamoja na kuimarisha malezi yenye maadili, usawa na uwajibikaji wa pamoja ili kujenga jamii salama na yenye kuheshimu utu wa kila mmoja.





Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.