Amana Hospitali Yaadhimisha Siku ya Kinywa na Meno kwa Kutoa Huduma Bure.
Hospitali ya Amana leo imeungana na dunia nzima kuadhimisha Siku ya Kinywa na Meno Duniani yenye kaulimbiu “Kinywa Chenye Furaha, Fikra Tulivu” kwa kutoa huduma za bure za uchunguzi na matibabu ya meno kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Dkt. Elisia Mpango amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuhamasisha wananchi kutunza afya ya kinywa na kuelewa umuhimu wake katika maisha ya kila siku.
“Afya ya kinywa ni msingi wa afya bora kwa ujumla. Watu wengi hupuuza matatizo ya meno bila kujua kuwa yanaweza kusababisha maumivu makali, matatizo ya lishe, na hata kuathiri afya ya akili. Kupitia huduma hizi za bure, tunataka kuwaelimisha wananchi na kuwapa fursa ya kupata matibabu mapema,” amesema Dkt. Mpango
Kwa upande wake Daktari bingwa wa kinywa na meno wa Amana Hospitali Dkt. Amimu Kilomoni amesema matatizo ya kinywa kama vile kuoza kwa meno na magonjwa ya fizi yanaweza kuzuilika kwa kufuata kanuni bora za usafi wa kinywa, ikiwemo kupiga mswaki mara mbili kwa siku kwa kutumia dawa yenye floridi, kuepuka vyakula vyenye sukari nyingi, na kutembelea daktari wa meno mara kwa mara.
Nao Wananchi waliopata huduma katika hospitali hiyo wameeleza kufurahishwa na juhudi za Amana Hospitali katika kuimarisha afya ya jamii.
“Sikuwahi kufikiria kama tatizo langu la meno lingeweza kutatuliwa bure. Leo nimepata uchunguzi na ushauri wa daktari wa meno, na pia nimejifunza jinsi ya kutunza meno yangu vyema,” alisema Bi. Amina Juma, mmoja wa wakazi wa Ilala aliyefika kupata huduma.
Katika maadhimisho hayo, mamia ya wananchi wamejitokeza kupata huduma mbalimbali za afya ya kinywa, ikiwemo uchunguzi wa matatizo ya fizi na meno na ushauri wa kiafya kutoka kwa madaktari bingwa wa meno wa hospitali hiyo.
Hata hivyo Amana hospitali imeahidi kuendeleza kampeni za elimu na huduma za afya ya kinywa ili kuhakikisha wananchi wanapata matibabu stahiki na kuimarisha afya zao kwa ujumla.

Comments
Post a Comment