Asasi za kiraia zimelaani tukio la kifo cha mwanafunzi kilichosababishwa na adhabu ya viboko iliyotolewa na mwalimu wake.

 


Asasi za kiraia vinara wa upingaji wa adhabu za ukatili shuleni, zimelaani na kukemea tukio la kifo cha mwanafunzi wa kidato cha pili Mhoja Maduhu kutoka shule ya sekondari Mwasamba Kata ya Lutubiga Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu kilichosababishwa na adhabu ya viboko iliyotolewa na mwalimu wake February 26 mwaka huu.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Asasi washirika,Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HakiElimu Dkt. John Kalaghe amesema tukio hilo linakiuka miongozo ya utolewaji wa adhabu za viboko shuleni na linaendeleza vitendo vya ukatili kwa watoto shuleni na kufifisha mazingira salama ya kujifunza na utolewaji wa elimu hapa nchini.


Aidha Dkt Kalaghe amesema wanasikitika kuona matukio kama hayo yakiendelea kujitokeza licha ya hatua za kisheria kuchukuliwa kwa walimu husika kwani tukio hilo linafanana na tukuo la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius la mwaka 2018 aliyekua anasoma shule ya Msingi Kibeta,Manispaa ya Bukoba ambaye alifariki kutokana na adhabu ya viboko kutoka kwa walimu wake.


Amesema kwa mujibu wa utafiti wa Hakielimu wa Mwaka 2020 unaonyesha kuwa kuna matukio mengi mashuleni ambapo takribani asilimia 87.9 ya wanafunzi waliripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 90 ya hao waliripoti kuwa ukatili huo waliofanyiwa ulitokana na adhabu za viboko toka kwa walimu wao na asilimia 10 walifanyiwa nyumbani.



Kwa upande wake meneja programu wa Shirika la Children in Crossfire, Saraphina Lelo amesema licha ya aina hiyo ya ukatili kufanyika zaidi shuleni, ipo hatari ya kuendelea kutengeneza jamii yenye vitendo vya ukatili.


"Ikumbukwe huyu mtoto ndiye atakuja kuwa baba au mama hivyo anaweza kuendeleza adhabu hiyo kwa watoto wake,Jamii itaendelea ikijua viboko ndiyo adhabu sahihi kwa mtoto wakati inamuumiza," amesema Saraphina.


Kutokana na matukio hayo Asasi za kiraia zimetoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za kukomesha kabisa matumizi ya adhabu ya viboko shuleni na kuhimiza adhabu chanya au adhabu mbadala ambazo sio za kikatili zinazohimiza nidhamu kwa wanafunzi.


Tamko hilo Limetolewa na Mashirika Vinara wa Upingaji wa adhabu za kikatili Shuleni ambayo ni pamoja na HakiElimu,Save the Children,Msichana Initiative ,TCRF na CIC. 





Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.