Serikali yatenga Sh.Billion 450 kwaajili ya kujenga Arena.
SERIKALI imesema itajenga Arena yenye uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 15,000 katika eneo la Kawe Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambae pia ni Msemaji wa Serikali Gerson Msigwa amesema baada ya Rais Samia kufanya ziara Korea, amepata mkopo wa masharti nafuu wa Dola bilioni 2.5.
“Kati ya fedha hizo ameamua kukata Sh bilioni 450 kwa ajili ya kuzileta Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujenga Arena kwanza halafu itafuatia kijiji cha filamu,”amesema.
Amesema fedha zitakapotoka Korea na kufika kwao wataanza ujenzi wa Arena mara moja ili uwanja huo uanze kutumika kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani.
“Ndugu zangu wasanii tumshukuru sana Rais Samia, hili jambo lilikuwa linamuumiza kichwa hivyo pesa alizotoa tutajenga pale Kawe Arena hiyo”amesema Msigwa.
Msigwa amesema uwanja huo utakuwa unatumika kwa shughuli nyingine mbalimbali ikiwemo maombi ya kitaifa, mashindano ya Quran na mambo mengine ya kijamii na kitaifa.
Amesema Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) hawapendezwi wanavyotumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya shughuli za nje ya mchezo wa mpira wa miguu katika uwanja huo.
“Inawaudhi kwasababu wanaona viwango vya ubora wa uwanja vinaharibiwa. Lakini kwasababu hatuna mahali pengine pa kufanyia shughuli hizi, Arena itasaidia kuondokana na haya,”amesema Msigwa.

Comments
Post a Comment