DC Edward Mpogolo:Rais Samia ametoa bilioni 32 kwaajili ya sekta ya elimu Ilala.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, ametoa zaidi ya Bilioni 32 kwaajili ya sekta ya Elimu katika idara ya elimu sekondari wilayani Ilala.
Mheshimiwa Edward Mpogolo ,alisema hayo wakati wa ziara yake kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo shule ya sekondari Kitunda ambayo imegharimu shilingi bilioni 4.6.
“Dkt.Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa fedha zaidi ya shilingi bilioni 32 kwa ajili ya miundombinu ya elimu idara ya Elimu Sekondari wilaya yetu ya Ilala tunamshukuru sana tunaunga mkono juhudi zake za utekelezaji wa Ilani”alisema Mpogolo.
Mpogolo alisema fedha hizo zimetokana na Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo yamekuwa chagizo kwa ajili ya ujenzi wa shule za Sekondari za magorofa.
Aidha alisema sasa hivi Halmashauri inakwenda kuonyesha nguvu ya ukusanyaji wa fedha kwa ujenzi wa shule za kisasa ambapo shule hiyo ya Kitunda itakuwa ya ghorofa nne,madarasa 16,maktaba ya kisasa ,mahabara 4 na Ofisi 12 .
Alitumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya, kwa uchapakazi wake kwa ajili ya kusimamia miradi ya maendeleo vizuri.
Wakati huo huo alitoa agizo kwa Mkurugenzi wa jiji Elihuruma Mabelya, kuhakikisha Mkandarasi wa ujenzi huo wa shule ya sekondari anakamilisha kwa wakati ujenzi wa shule hiyo mpaka February 2026 iwe imekamilika ili Wanafunzi wa shule za Serikali za Kitunda ,Kivule, Ukonga,Kipawa na Kipunguni waweze kusoma katika shule hiyo ya kisasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam Elihuruma Mabelya,alisema mradi huo wa shule ya sekondari kitunda utakuwa manufaa makubwa kwa wananchi na utawawezesha kutatua changamoto za mrundikano wanafunzi madarasani mradi ambao kwa sasa upo katika hatua ya ujenzi wa gorofa moja.




Comments
Post a Comment