NIDA yatangaza kusitisha matumizi ya namba za vitambulisho kwa wasiovichukua kufikia Mei Mosi, 2025.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha vitambulisho vinatolewa kwa walio tayari kuvipokea, baada ya kubainika kuwa idadi kubwa ya wananchi hawakufika ofisini licha ya kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kuwajulisha kwenda kuchukua vitambulisho vyao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mapema April 14,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji ambapo alisema kuwa kati ya wananchi 1,880,608 waliotumiwa SMS kati ya Januari na Machi 23, 2025, ni 565,876 pekee waliokwenda kuchukua vitambulisho hivyo, sawa na asilimia 30.
“NIDA imesikitishwa na mwitikio mdogo wa wananchi licha ya kufahamishwa rasmi. Hivyo, kuanzia Mei Mosi, tutasitisha matumizi ya namba kwa wale wote ambao hawajajitokeza,” alisema Kaji.
Kaji alibainisha kuwa tangu kuanza kwa zoezi hilo mapema Januari mwaka huu, jumla ya ujumbe 1,880,608 zilitumwa kwa waombaji, ikiwa ni sawa na asilimia 157 ya vitambulisho 1.2 milioni vilivyokuwa havijachukuliwa kutoka kwa ofisi za kata, vijiji na mitaa.
“Kati ya SMS hizo, 680,608 zilitumwa kwa waombaji wapya ambao vitambulisho vyao vimechapishwa na vinangojea kuchukuliwa,” alieleza Kaji.
Kwa mujibu wa Kaji, mfumo mpya wa utoaji vitambulisho unalenga kuongeza ufanisi kwa kuanzisha muda maalum wa kuchukua vitambulisho.
Alisema baada ya kusajiliwa, mwombaji atapokea namba ya NIDA ndani ya siku tano, na ndani ya siku 21, atapokea ujumbe mwingine wa kumwelekeza mahali pa kuchukua kitambulisho na iwapo atashindwa kufanya hivyo ndani ya mwezi mmoja, namba yake ya NIDA itafutwa.
“Tunawahimiza wananchi kutunza ujumbe na kufika ofisini mapema ili kuepusha usumbufu na madhara ya kutopata huduma zinazotegemea kitambulisho hiki,” alisema.
Kaji alisema kuwa NIDA inatafakari uwezekano wa kuweka faini kwa wananchi watakaokaidi utaratibu huo, ikizingatiwa kuwa serikali inatumia rasilimali kubwa kutoa huduma hiyo bila malipo.
Aidha, aliwataka vijana wanaotimiza miaka 18 kuanza kujisajili mapema badala ya kungoja hadi wanapotafuta ajira, hali inayosababisha msongamano na migongano isiyo ya lazima kwenye ofisi za NIDA.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri mwenye dhamana, Kaji alisema kuwa kila ofisi ya NIDA nchini sasa itakuwa na afisa kutoka Idara ya Uhamiaji ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kuhusu vitambulisho vilivyokuwa vimefutika, Kaji alisema serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imeanza kutoa vitambulisho vipya kwa wananchi waliokumbwa na changamoto hiyo. Alisisitiza umuhimu wa kujaza fomu kwa usahihi ili kuepuka makosa ya majina na taarifa nyingine muhimu.
Akizungumzia taarifa zinazosambaa mitandaoni kuwa NIDA inahusika na usajili wa bima ya Toto Afya Card, Kaji alikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa NIDA haina jukumu lolote kwenye mpango huo wa bima.
Katika hatua nyingine, NIDA imetangaza kuanza kwa mpango wa utambuzi na usajili wa watu wote walio chini ya miaka 18, pamoja na raia wa kigeni wanaoingia nchini na kukaa zaidi ya miezi sita, ambao wote watapatiwa jamii namba.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, zoezi hilo litaanza kwa majaribio katika wilaya za Kusini-Kusini (Unguja), Kilolo (Iringa) na Rungwe (Mbeya), ambapo zaidi ya watu 335,826 wanatarajiwa kufikiwa katika kipindi cha miezi miwili.
NIDA inasisitiza kuwa kuchukua kitambulisho cha Taifa ni haki na pia wajibu wa kila raia, kwani ndicho msingi wa kupata huduma muhimu kama vile benki, ajira, elimu, afya, mawasiliano na huduma nyingine za kijamii na kiuchumi.


Comments
Post a Comment