RAIS SAMIA ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 4,887 KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 61 YA MUUNGANO.

Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametumia mamlaka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1) (a)-(d) ya Katiba na kutoa msamaha kwa makundi mbalimbali ya wafungwa nchini.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, msamaha huo umewahusu wafungwa waliotimiza vigezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kupunguziwa sehemu ya vifungo vyao, kuondolewa kabisa kifungo, au kubadilishiwa adhabu.


 Jumla ya wafungwa 4,887 wamenufaika na msamaha huo, ambapo 42 kati yao wameachiliwa huru mara moja na wengine 4,845 wataendelea kutumikia sehemu iliyobaki ya vifungo vyao baada ya msamaha huo.


Miongoni mwa waliopata msamaha ni:


  • Wafungwa waliopunguziwa sehemu ya vifungo vyao.
  • Wafungwa wagonjwa sugu walioko hatua ya mwisho ya ugonjwa.
  • Wafungwa wa maisha waliobadilishiwa vifungo vyao kuwa miaka 30.
  • Wafungwa waliokadiriwa kunyongwa waliobadilishiwa adhabu kuwa kifungo cha maisha.
  • Wazee wa miaka 70 au zaidi waliokaa gerezani kwa angalau miaka miwili.
  • Wafungwa wa kike walioko gerezani wakiwa na mimba au watoto wachanga.
  • Wafungwa wenye ulemavu wa mwili au akili waliothibitishwa na jopo la madaktari.



Hata hivyo, msamaha huo haukuwahusu wafungwa wa makosa makubwa kama vile uhujumu uchumi, rushwa, utakatishaji fedha, makosa dhidi ya watoto, biashara ya binadamu, ujangili, ugaidi, na uhalifu wa kimtandao, miongoni mwa mengine.


Serikali imetoa wito kwa wafungwa waliopata msamaha kutumia fursa hiyo kujirekebisha na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa, huku wakiepuka kujihusisha na makosa ambayo yangeweza kuwarejesha tena gerezani.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.