RC CHALAMILA AZINDUA UTOAJI WA MIKOPO YA 10% MANISPAA YA TEMEKE.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, leo Aprili 24, 2025, amezindua rasmi utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke. 


Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga, Jijini Dar es Salaam.


Akihutubia katika hafla hiyo, Mhe. Chalamila amesema kuwa mikopo hiyo isiyokuwa na riba ni jitihada mahsusi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wakazi wa Wilaya ya Temeke.


“Lazima mikopo hii irejeshwe kwa wakati ili na wengine wapate fursa ya kunufaika,” alisisitiza Chalamila.


Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wananchi kuacha tabia ya kulaumu Serikali badala yake watumie changamoto kama daraja la mafanikio. 


“Unakuta mtu anatoka Kigoma pembezoni, anakuja mjini, anauza madafu, kesho na keshokutwa anakuwa mfanyabiashara mkubwa. Lakini mzawa wa hapa Temeke kila siku analalamika Serikali,” alisema Chalamila.


Katika hatua nyingine, Mhe. Chalamila alitembelea mabanda mbalimbali ya wajasiriamali walionufaika na mikopo hiyo na kujionea bidhaa wanazozalisha ikiwa ni ishara ya mafanikio ya mpango huo.


Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Temeke, Mhe. Abdallah Mtinika, alimshukuru Rais Samia kwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo hiyo, akifafanua kuwa ucheleweshaji uliokuwepo hapo awali ulitokana na mchakato wa kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi ili kuhakikisha mikopo inarejeshwa kwa wakati.


“Mfumo bora sasa umewekwa, hivyo tunatarajia uwajibikaji zaidi kutoka kwa wanufaika,” alisema Meya Mtinika.


Mpango wa mikopo ya asilimia 10 ni utekelezaji wa sera ya Serikali kupitia halmashauri za wilaya, ambapo asilimia hiyo hutengwa kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha makundi maalum ya kijamii.



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.