Steve Nyerere Atoa Wito kwa Viongozi wa Dini Kuepuka Siasa Katika Nyumba za Ibada.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Mengele maarufu kama Steve Nyerere, amewaasa viongozi wa dini kuhakikisha wanahimiza amani na upendo katika nyumba za ibada, badala ya kupandikiza chuki za kisiasa kwa waumini wao, ili kudumisha amani iliyopo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Steve alisema kuwa viongozi wa dini wana wajibu mkubwa wa kuitunza amani ya taifa, hivyo wanapaswa kuepuka tabia ya kueneza chuki au kutoa hotuba zenye mwelekeo wa kisiasa mbele ya waumini.
“Viongozi wa dini wanaoingiza siasa za uchochezi kwenye nyumba za ibada, ni vyema wakaweka wazi kwamba wameamua kuingia kwenye siasa, badala ya kuhubiri neno la Mungu. Wajiweke wazi tu, tutawaelewa,” alisema Steve.
Aliongeza kuwa viongozi wa dini wanapaswa kubaki kwenye jukumu lao la kufundisha maadili mema kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Mambo ya kisiasa, alisema, waachie wanasiasa, ambao nao wanapaswa kufanya siasa safi zisizogawa jamii.
“Tunalinda taifa letu kwa maslahi yetu sote. Tusikubali watu wachache kutuharibia amani. Zamani kulikuwepo na utaratibu wa kuwaombea viongozi wetu, wanafunzi, na taifa kwa ujumla, lakini siku hizi utaratibu huo umetoweka; muda mwingi hutumika kuhubiri siasa,” alisisitiza.
“Viongozi wa kiroho warudi katika misingi ya awali, ambapo nyumba za ibada zilikuwa sehemu ya kupata amani ya moyo. Leo hii, tuna matatizo mengi yanayohitaji maombi, lakini mtu akiingia kuswali, anatumia dakika tano tu, huku mahubiri ya siasa yakichukua zaidi ya dakika 70. Hii si sahihi,” alieleza.
Amehitimisha kwa kusema kuwa nyumba za ibada zinapaswa kuwa mahali pa kumuomba Mungu na kusaidia watu kupata nafuu ya kiroho na kimaisha, badala ya kuwa majukwaa ya kisiasa.



Comments
Post a Comment