Papa Mpya Atangazwa Rasmi: Kardinali Robert Prevost Achaguliwa Kuwa Papa Leo XIV.


Kardinali Robert Prevost, mzaliwa wa Chicago, Marekani, ametangazwa rasmi kuwa kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani na atajulikana kwa jina la Papa Leo XIV.


Papa Leo XIV mwenye umri wa miaka 69, alihudumu hadi hivi karibuni kama Mkuu wa Dicastery ya Maaskofu katika Vatican. Pamoja na kuwa raia wa Marekani, Papa huyu mpya pia ana uraia wa Peru, ambako amehudumu kwa muda mrefu katika shughuli za kichungaji.


Akihutubia maelfu ya waumini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kwa mara yake ya kwanza kama Papa, alitoa ujumbe wa matumaini na amani:

“Amani iwe nanyi nyote. Wapendwa, ndugu na kina dada, hii ni salamu ya kwanza ya ufufuko wa Kristo. Ningependa kutoa salamu ya amani iwafikie familia zenu, ninyi nyote, popote mlipo. Amani iwe nanyi.”



Uchaguzi huu unafuatia kifo cha Papa Francis aliyefariki dunia Jumatatu ya Pasaka tarehe 21 Aprili akiwa na umri wa miaka 88. Mazishi yake yalifanyika Jumamosi tarehe 26 Aprili na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka kote duniani.


Mkutano wa siri wa uchaguzi wa Papa (Conclave) ulianza jana katika Kanisa dogo la Sistina, ambapo makardinali 133 kutoka duniani kote walishiriki. Huu ni mkutano wa tatu mfululizo wa uchaguzi wa Papa kufanyika ndani ya siku mbili, kama ilivyokuwa mwaka 2005 na 2013.


Kabla ya kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV, kulikuwa na majina kadhaa yaliyokuwa yakitajwa kama warithi wa kiti cha Mtakatifu Petro.

Kati ya waliotajwa sana ni Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu wa Mambo ya Nje wa Vatican; Kardinali Peter Turkson kutoka Ghana; Kardinali Fridolin Ambongo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Kardinali Luis Antonio Tagle wa Ufilipino; pamoja na Kardinali Joseph Tobin na Prevost mwenyewe.


Kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV kunatazamwa kama mwelekeo mpya wa uongozi wa Kanisa Katoliki duniani, ukionesha muunganiko wa uzoefu wa kichungaji, utawala wa Kanisa, na maono ya kimataifa.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.