Ndoa za Utotoni Zikome: Wadau Wanena kwa Sauti Moja.


Na Fidea Masunga,Dar es Salaam


Katika harakati za kulinda haki za mtoto wa kike na kuhakikisha ndoto zao hazikatizwi mapema, Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN) umefanya kikao maaalum cha kuthibitisha Mpango Mkakati wa Uchechemuzi na Mawasiliano kitakachotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu.


Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam kimewakutanisha wadau kutoka mashirika ya kiraia, taasisi za kiserikali, viongozi wa dini pamoja na watoto wenyewe,sauti ambazo mara nyingi hazisikiki kwenye meza za maamuzi.


Adeline na Adela, watoto wawili waliokuwa miongoni mwa washiriki, walitoa ushuhuda wa kugusa moyo kuhusu madhila ya ndoa za utotoni ambaoo Walisema watoto wengi hupoteza mwelekeo wa maisha kutokana na kuozeshwa mapema, huku wakiomba serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wazazi wanaoruhusu vitendo hivyo.


“Tunaomba tulindwe. Tunataka kusoma, sio kuolewa,” alisema Adela.


Nae mtoto Adeline aliiomba serikali na wanaharakati mbalimbali wakutetea haki za watoto kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa jamii ili kuweza kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni na kukomboa kizazi cha sasa na kile kijacho.


Bi. Amina Ally kutoka shirika la My Legacy ambao ni miongoni mwa shirika wanachama  wa TECMN alisema kuwa mpango kazi huo mpya unalenga kuwafikia zaidi ya Watanzania milioni tano kupitia kampeni za kitaifa, elimu kwa jamii, na ushawishi wa sera.

“Hatutaki kupaza sauti tu, tunataka mabadiliko ya kweli kwenye sheria na maisha ya watoto vijijini,” alisisitiza.


Mratibu wa TECMN, Bi. Lilian Kimati, alibainisha kuwa moja ya maeneo ya kipaumbele ni kushawishi maboresho katika Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, ambayo bado inaruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa chini ya miaka 18 kwa ridhaa ya wazazi au mahakama.


“Sheria hii ni ya zamani, haiendani na wakati. Haki ya mtoto lazima ilindwe kisera na kisheria,” alisema Kimati.


Mpango huu wa miaka mitatu unatarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni na unatazamwa kuwa nyenzo madhubuti ya kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watoto wa kike nchini Tanzania.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.