CCM Yavunja Rekodi ya Uchukuaji Fomu, Zaidi ya 20,000 Wajitokeza Kugombea Nafasi za Ubunge na Udiwani.


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza kukamilisha kwa mafanikio makubwa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, huku zaidi ya wanachama 20,000wakijitokeza kuwania nafasi hizo.


Zoezi hilo lilianza tarehe 28 Juni na kukamilika rasmi Julai 2, likihusisha nafasi za Udiwani, Ubunge, Uwakilishi, pamoja na Viti Maalum kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Amos Makalla, alisema kuwa idadi hiyo kubwa ya waombaji ni ishara tosha kuwa CCM bado kinaaminiwa sana na Watanzania wa makundi yote.


“Tumevunjwa rekodi. Hamasa imekuwa kubwa kuliko wakati wowote wa nyuma. Tumeshuhudia makundi mbalimbali yakijitokeza kwa wingi vijana, wanawake, wasanii, bodaboda, machinga, wakulima na wengineo. Hii ni dalili kuwa CCM ni chama imara, chenye sera thabiti na matumaini ya Watanzania,” alisema Makalla.


Aidha Makalla alisema Takwimu Kuu za Uchukuaji Fomu kwa Tanzania Bara jumla ya Waombaji 1,163 walichukua fomu za ubunge katika majimbo 273 ambapo Zanzibar Waombaji walikua 84 katika majimbo 54 huku upande wa Uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu walikua 83.


Kwa upande wa Udiwani takribani waombaji 15,000 walijitokeza kwenye kata 3,960,upande wa UWT walikua ni 123 (Bara), 8 (Zanzibar), na 9 wa viti maalum.


Aliongeza kuwa UVCCM walikua 154 (Bara), 7 (Zanzibar) ambapo jumla ni 161 huku upande wa Jumuiya ya Wazaziwalikua 62 kwa ubunge na uwakilishi.


“Kwa ujumla kupitia takwimu hiyo wanachama waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali wanakadiriwa kufikia zaidi ya 20,000, idadi ambayo haijawahi kufikiwa hapo awali katika historia ya CCM” alisema Makalla


Hata hivyo kwa mujibu wa Makalla, vikao vya uteuzi vinaanza rasmi Julai 4, kuanzia ngazi ya kata kwa wagombea wa udiwani, na kufuatiwa na vikao vya mikoa tarehe 9 Julai


Kwa upande wa ubunge na uwakilishi, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itafanya uteuzi wa mwisho tarehe 19 Julai 2025.


Alisema Katika mfumo mpya wa uteuzi, chama hicho kitaainisha wagombea watatu bora kwa kila nafasi kabla ya kupitishwa rasmi na vikao vya juu, tofauti na mfumo wa zamani ambapo wagombea walienda moja kwa moja kupigiwa kura.


“Tunataka wagombea bora, waadilifu na wanaokubalika kwa wananchi. Mfumo huu unalenga kuongeza ubora wa viongozi wanaopitishwa na CCM,” alisisitiza Makalla.


Makalla alisema Mwenyekiti wa CCM Dkt Samia Suluhu Hassan amevitaka vikao vya uchujaji vitende haki visionee watu na haki ionekane ikitendeka na kuwaomba  wanachama kuwa watulivu wakati wa mchakato wa uteuzi ndani ya chama.


“Nimeelekezwa kwa niaba ya Halmashauri Kuu ya Taifa Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt Samia Suluhu Hassan anavitaka vikao vya uchujaji vitende haki visionee watu, vitende haki na haki ionekane ikitendeka,” amesema Makalla.


“Tunatambua kiu yao ya kutaka kuhudumu kwa wananchi kupitia CCM. Hata hivyo, ni muhimu kusubiri maamuzi ya chama kwa nidhamu na subira,” aliongeza.



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.