DCP MISIME AWATAKA POLISI KATA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI NA USHIRIKIANO KATIKA KATA ZAO.
Msemaji wa Jeshi la Polisi Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime amewataka Polisi Kata kuzingatia maadili na kushirikiana na Viongozi wa Serikali za Mitaa waliopo katika maeneo yao ili kuhakikisha wanatekeleza kwa usahihi misingi ya uanzishwaji wa falsafa ya Polisi Jamii kwa kuhakikisha wanabaini, wanazuia na kutanzua uhalifu katika maeneo yao.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 25, 2025 alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kuzungumza na Maafisa wa Polisi Jamii na Polisi Kata wa Kanda Maalum Dar es salaam katika ukumbi wa bwalo la Polisi barabara ya Kilwa Temeke Dar es salaam.
DCP Misime amesema " Jukumu lako wewe Polisi Kata ni kujenga na kuimarisha ushirikiano na maadili katika Kata yako kwa kuhakikisha mnashirikiana vizuri na Viongozi wa Serikali na kufanya kazi kwa kuzingatia kauli mbiu ya Jeshi letu la Polisi ya nidhamu haki weledi na uadilifu".
DCP Misime alipata fursa ya kufafanua maudhui yaliyomo katika kitabu cha mwongozo wa mafunzo ya Polisi Kata chenye lengo la kuhakikisha Polisi Kata wote nchini wanakuwa na mfanano wa nini kinatakiwa kuwasilishwa kwa jamii juu ya ushirikishwaji wa jamii katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu katika jamii husika.
Pia Afisa Mnadhimu wa Kamisheni ya Polisi Jamii Makao Makuu ya Polisi Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) George Salala alifafanua majukumu ya Polisi Kata na Viongozi wa Serikali za Mitaa katika kuhakikisha jamii yao inakuwa salama muda wote.
Aidha, kwa upande wake Mkaguzi wa Polisi Agness Mwayombo kutoka Makao Makuu ya Polisi alisisitiza kutoa kipaumbele kwa uwasilishaji wa mada za ukatili wa kijinsia kwa jamii sambamba na kuwahudumia mahanga na manusula katika mazingira yenye kuzingatia utulivu na usiri.
Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Kanda Maalum Dar es salaam Kamishna Msaidizi wa Polisi Leah Mbunda amewashukuru wawasilishaji mada wote kwa mada zao nzuri zenye kuleta tija katika ufanyaji wa kazi za Polisi.



Comments
Post a Comment