“Kuna Maisha Baada ya Uchaguzi, Tuwe Mabalozi wa Amani”-Jaji Mutungi.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amevitaka vyama vya siasa kufanya kampeni za kistaarabu na kuepuka lugha zinazoweza kuhatarisha amani ya taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa vyama, Jaji Mutungi alisema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa namna sheria hiyo inavyotekelezwa ili kuepusha kasoro kwenye uchaguzi.
“Kuna maisha baada ya uchaguzi. Amani ya Taifa ipewe kipaumbele. Tukitumbukia kwenye machafuko, hatutakuwa na siasa wala maendeleo,” alisema Jaji Mutungi.
Aidha, aliwataka wagombea kuja na sera bora zitakazowashawishi wananchi badala ya kushindana kwa lugha za matusi dhidi ya wenzao huku akionya kuhusu taarifa za upotoshaji mitandaoni akisisitiza kwamba uvumi wa kutokuwepo uchaguzi hauna msingi.
“Uchaguzi upo, na utakuwa wa amani na haki,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu, aliwahimiza wagombea na vyama kuzingatia masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ili kuepusha makosa ya kisheria.
Awali Khatibu amempongeza msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa hatua ya kuwaleta pamoja viongozi wa kitaifa na watendaji wa vyama kwa lengo la kutoa elimu na kuimarisha msingi wa demokrasia.
"Mheshimiwa mgeni rasmi, tunakupongeza sana kwa kazi nzuri ya ulezi wa vyama vya siasa. Umeona umuhimu wa kutukutanisha hapa ili kupitia sheria ya gharama za uchaguzi, jambo hili ni jema kwa sababu linapunguza kasoro katika uchaguzi wetu," alisema Khatibu.
“Awali baadhi ya wagombea walikuwa hawana uelewa wa kutosha na walijikuta wakitumia risiti za kughushi wakidhani watarudishiwa fedha. Leo tunapata elimu ya kutosha,” aliongeza Khatibu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema fomu na nyaraka zinazotolewa kwa Kiingereza zinawapa changamoto kubwa wagombea wengi.
“Wagombea wengi wanafahamu Kiswahili vizuri zaidi. Tukipata fomu na nyaraka kwa Kiswahili itarahisisha uelewa na kupunguza makosa,” alisema Profesa Lipumba.
Aidha, aliongeza kuwa sharti la mgombea kuwa na akaunti ya benki binafsi linaweza kuwa kikwazo kwa baadhi ya wagombea wa maeneo ya pembezoni ambako huduma hizo hazijafika kwa urahisi.
Kwa upande wake, Mgombea Urais wa Chama cha NLD, Doyo Hassan, alisema fomu za Kiingereza zinawatenga wagombea wasioweza lugha hiyo, jambo linalowalazimisha kujaza fomu chini ya msaada wa watu wengine.
“Hali hii inaweza kuathiri uhuru na usahihi wa taarifa za mgombea,” alisema Doyo.
Mafunzo hayo yamelenga kusaidia vyama na wagombea kuendesha kampeni kwa uwazi, uadilifu na bila migogoro, huku washiriki wakisisitiza umuhimu wa kutumia Kiswahili ili sheria iweze kueleweka kwa kila mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.


Comments
Post a Comment