Mpina, Mluumbe waenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha urais
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetengua uteuzi wa wagombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliokuwa wamepitishwa na vyama vyao.
Wagombea waliotenguliwa ni Bw. Wilson Elias Mluumbe wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) na Bw. Luhaga Joelson Mpina wa ACT–Wazalendo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msajili, imesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kupitia vielelezo na ushahidi uliowasilishwa na pande husika, na kubaini kuwa mchakato wa uteuzi ndani ya vyama hivyo ulikiuka Sheria ya Vyama vya Siasa (Sura 258), pamoja na Katiba na Kanuni za vyama husika.
Msajili amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa kifungu cha 6A(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vinapaswa kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia Katiba ya Nchi, Sheria, pamoja na Katiba na Kanuni zao.
Aidha, alionya kuwa wagombea wa nafasi mbalimbali lazima wapitishwe kwa njia halali na ya kidemokrasia ili kulinda utawala wa sheria, amani na mshikamano wa kitaifa.
Vyama husika vimepewa barua rasmi kuhusu uamuzi huo na kuagizwa kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria. Wakati huo huo, Msajili ameushukuru ushirikiano wa vyama hivyo katika kushughulikia malalamiko yaliyowasilishwa.
Pamoja na hilo, Msajili amevikumbusha vyama vyote vyenye usajili kamili kuendelea kuzingatia sheria, Katiba na misingi ya demokrasia kabla, wakati na baada ya uchaguzi.


Comments
Post a Comment