Doyo Hassan Doyo Akidhi Vigezo vya Uteuzi, NLD Yashukuru Wananchi.
Chama cha National League for Democracy (NLD) kimeeleza shukrani zake kwa wananchi waliojitokeza kwa wingi katika mikoa 10 ya Tanzania Bara na Visiwani kumdhamini Mheshimiwa Doyo Hassan Doyo, mgombea wake wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Zoezi la kukusanya wadhamini lilianza rasmi tarehe 10 Agosti 2025, mara baada ya Doyo kuchukua fomu ya uteuzi ambapo zoezi hilo limehitimishwa rasmi leo, 22 Agosti 2025 jijini Dar es Salaam.
Vilevile Mh.Doyo alikamilisha kiapo chake katika Mahakama Kuu ya Tanzania, hatua inayomwezesha kuendelea na mchakato wa uteuzi.
Mgombea huyo wa Urais wa NLD anatarajia kurudisha fomu ya uteuzi rasmi tarehe 24 Agosti 2025, jijini Dodoma, kisha kusubiri uamuzi wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Akizungumza kwa niaba ya chama, Don Waziri Mnyamani, Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Taifa, NLD, alisema kuwa chama kinathamini moyo wa uzalendo, mshikamano na imani iliyoneshwa na wananchi katika hatua hii muhimu ya kisiasa.
Aliongeza kuwa NLD itaendelea kusimama imara kwa maslahi ya wananchi na maendeleo ya kweli ya Tanzania.

Comments
Post a Comment