ASKARI MAGEREZA AFARIKI NJOMBE BAADA YA KUJIRUSHA KWENYE GARI LA POLISI.
Askari wa Jeshi la Magereza mkoani Njombe, Erasto Mlelwa (26) mwenye namba C.916 WDR, amefariki dunia baada ya kujirusha kutoka ndani ya gari la Polisi lililokuwa kwenye mwendo, akidaiwa kufanya hivyo mara baada ya kuoneshwa mwili wa askari mwenzake anayedaiwa kumuua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa Mlelwa alijirusha kutoka kwenye gari wakati Jeshi la Polisi likielekea Hospitali ya Lilondo, Madaba mkoani Ruvuma kwa ajili ya uchunguzi wa mwili wa askari huyo aliyeuawa.
“Mtuhumiwa baada ya kuona mambo yako wazi aliamua kujitoa uhai wake kwa kuruka kutoka kwenye gari na kuangukia kichwa. Alipofikishwa hospitali tayari alikuwa amepoteza maisha,” alisema RPC Banga.
RPC Banga alifafanua kuwa, Jeshi la Polisi lilikuwa likiendelea na uchunguzi wa kupotea kwa Askari Magereza C.681 WDR Dickraka Mwamakula (24) tangu Septemba 7, 2025, ambapo kwa mara ya mwisho alionekana akiwa na Mlelwa katika eneo la Lilondo kwa shughuli za mashamba.
Baada ya msako na uchunguzi, mwili wa Mwamakula ulipatikana umefukiwa shambani, ukiwa na jeraha kisogoni na kuchomwa moto.
Polisi wamesema chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni wivu wa kikazi, baada ya Mlelwa kudaiwa kutoridhishwa na namna Mwamakula alivyokuwa akipongezwa kutokana na utendaji wake.

Comments
Post a Comment