Biteko: Motisha kwa Wahandisi Ndiyo Nguvu ya Maendeleo ya Taifa.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema zaidi ya asilimia 70 ya ubunifu mpya wa kiteknolojia duniani unatokana na taaluma ya uhandisi, hivyo Serikali itaendelea kuwapa motisha wahandisi ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa.
Dkt. Biteko aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, alipomwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kufungua maadhimisho ya 22 ya Siku ya Wahandisi Tanzania, yaliyozinduliwa kwa kauli mbiu “Wajibu wa Wahandisi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 90 ya maendeleo ya viwanda duniani yanategemea huduma za wahandisi, hivyo ni taaluma isiyoweza kuepukika katika safari ya maendeleo ya taifa lolote.
“Kwa niaba ya Serikali, naomba niwakumbushe kuwa Taifa linawategemea sana.Tunawategemea, tunawahitaji, naomba mjue Serikali itaendelea kuwategemea wakati wote mnapotekeleza majukumu yenu,” alisema Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa motisha kwa wahandisi wanaoshiriki katika miradi ya kimkakati, sambamba na kuwajengea uwezo wa kushiriki miradi mingine, ni nyenzo muhimu ya kuimarisha kizazi cha wahandisi wazalendo.
Alisisitiza kuwa ERB haitakiwi kuishia kutoa adhabu pekee, bali pia ihakikishe inatambua na kupongeza wale wanaofanya vizuri kwa kuwatunuku zawadi na tuzo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alisema Wizara yake kwa kushirikiana na ERB itaendelea kuboresha mazingira ya kitaaluma kwa wahandisi, ikiwemo kuwapa mafunzo kwa vitendo kupitia mpango wa wahitimu (SEAP).
Alibainisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha wahandisi wazawa wanashiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati ya Taifa, ikiwemo ujenzi wa reli ya SGR, bomba la mafuta, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, pamoja na miradi ya maji na umeme.
“Tunataka kila mradi wa kimkakati uwe chuo cha vitendo kwa wahandisi wetu, ili ujuzi na utaalamu wa kizalendo uzidi kuimarika. Hii ndiyo njia pekee ya kuijengea nchi uwezo wa ndani wa kusimamia maendeleo yake,” alisema Ulega.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB),Mhandisi Wakili Menye Manga, alisema hadi sasa bodi imesajili wahandisi 44,000 na mafundi sanifu 3,445, lakini bado idadi hiyo haitoshelezi mahitaji ya nchi.
“ERB itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha idadi ya wahandisi inaongezeka sambamba na ubora wa taaluma hiyo”alisema Mhandisi Manga.
Maadhimisho ya mwaka huu yamehudhuriwa na zaidi ya wahandisi 4,000 kutoka ndani na nje ya nchi, ambapo mgeni rasmi alishuhudia kiapo cha wahandisi 400 na kuzindua ‘ERB Mhandisi App’ ambayo itawawezesha kupata taarifa mbalimbali za kitaaluma na kisheria nchini.





Comments
Post a Comment