Doyo: Nitaiunganisha Serengeti na Bunda, Arusha na Mikoa Mengine, Endapo NLD Itashinda.
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, ameahidi kuimarisha miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Serengeti, iwapo atachaguliwa kuwa Rais.
Akihutubia wakazi wa Mji wa Mugumu, Mhe. Doyo alisema ni aibu kwa wananchi wa Serengeti kukosa barabara za kisasa zinazowaunganisha na maeneo mengine, licha ya kuwa eneo hilo ni lango kuu la vivutio vya utalii nchini.
“Ni fedheha wananchi wa Serengeti kukosa barabara bora. Nitaunganisha Serengeti na Bunda, Arusha na mikoa mingine, ili mji huu uwe na tija kijamii na kukuza uchumi endelevu kwa vizazi vyenu,” alisema Mhe. Doyo.
Aliongeza kuwa baadhi ya mikoa ya Kaskazini tayari imenufaika na barabara za kiwango cha juu, jambo lililowarahisishia wananchi shughuli za biashara na maisha ya kila siku, hivyo wananchi wa Serengeti nao wanapaswa kufurahia maendeleo hayo.
Mhe. Doyo aliahidi kujenga barabara ya Zenge pamoja na miundombinu mingine muhimu, ili kuhakikisha Serengeti inapata kiunganishi cha kisasa chenye ubora na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.
Kwa sasa, msafara wa mgombea huyo wa NLD upo mkoani Mara kwa ajili ya kuanza rasmi kampeni katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.



Comments
Post a Comment