GCAP Yaitaka Serikali Kuchukua Hatua Madhubuti Kukabili Umasikini, Usawa na Changamoto za SDGs


Na Fidea Masunga,Dar es salaam.

Mtandao wa Kupambana na Umaskini (GCAP) Tanzania umeitaka Serikali kuchukua hatua za haraka na madhubuti kukabiliana na umasikini na ukosefu wa usawa nchini, ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote kwa usawa.


Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kuadhimisha miaka 10 ya utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs), Mratibu wa Taifa wa GCAP Tanzania, Martina M. Kabisama, alisema licha ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta za elimu, afya na miundombinu, bado kuna changamoto kubwa zinazohitaji suluhisho la dharura.


“Serikali isichukulie suala hili juu juu, bali ihakikishe sera na bajeti zinawalenga wananchi wote bila kubagua. Wapo wananchi wanaoendelea kusalia nyuma kutokana na umasikini, ukosefu wa usawa na athari za mabadiliko ya tabianchi,” alisema Kabisama.


Kwa upande wake, Rosemary Mwaipopo kutoka Dayspring Foundation, ambaye pia ni mwanachama wa GCAP, alisisitiza umuhimu wa Serikali kuongeza uwekezaji katika mifumo ya ulinzi wa kijamii na kupunguza pengo la usawa wa kijinsia na kiuchumi.


“Kila kaya inapaswa kupata kinga dhidi ya umasikini na mishtuko ya kiuchumi. Ajira zenye staha kwa vijana na wanawake ndizo msingi wa maendeleo jumuishi,” alisema Mwaipopo.


Katika tamko lake, GCAP ilibainisha changamoto saba kuu zinazozuia utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs) nchini. Changamoto hizo ni umasikini wa kipato, ajira duni kwa vijana na wanawake, ukosefu wa usawa wa kijinsia na kiuchumi, udhaifu wa mifumo ya uwajibikaji, athari za mabadiliko ya tabianchi, hifadhi ndogo ya kijamii pamoja na ukuaji wa uchumi usio jumuishi.


Mtandao huo ulisisitiza kuwa bila kushughulikia changamoto hizo kwa dhati, Tanzania inaweza kuchelewa kufikia Dira ya Maendeleo 2050 na kutimiza ajenda ya “maendeleo yasiyomwacha mtu nyuma” kama ilivyokusudiwa na SDGs.

.




 



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.