MAKAMU WA RAIS DKT. PHILIP MPANGO AKUTANA NA BALOZI MTEULE WA TANZANIA NCHINI JAPAN.


Dodoma, Tanzania – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Anderson Mutatembwa, katika kikao kilichofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.


Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais alisisitiza umuhimu wa diplomasia ya uchumi, akimtaka Balozi Mutatembwa kuhakikisha anavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Japan pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.


Amesema ni vema kushawishi makampuni ya Japan kuwekeza nchini Tanzania, hususan kwenye viwanda vya magari, dawa na vifaa tiba, bidhaa za kielektroniki pamoja na sekta ya lojistiki, kwa kuzingatia nafasi ya Tanzania kama lango la kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.


Aidha, Makamu wa Rais amemtaka Balozi Mutatembwa kuweka kipaumbele katika sekta za kimkakati ikiwemo Utalii, Kilimo, Uvuvi na Afya. Amesema Japan imepiga hatua kubwa katika teknolojia ya tiba ya magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo moyo na figo, hivyo ni vyema kuimarisha ushirikiano wa kitaaluma na tafiti kwa Watanzania.


Vilevile, Makamu wa Rais ameagiza kusimamiwa kwa makubaliano yaliyopo baina ya Tanzania na Japan kupitia Mpango wa Ushirikiano wa Japan na Afrika pamoja na mikataba ya ushirikiano kati ya miji ya nchi hizo mbili.


Amesisitiza pia umuhimu wa kuwaunganisha Watanzania wanaoishi nchini Japan ili kuchangia maendeleo ya Taifa, hususan kupitia uwekezaji katika sekta ya biashara na makazi, huku akiwakumbusha kuzingatia sheria na taratibu za nchi hiyo ili kulinda heshima ya Tanzania.


Pamoja na hayo, Makamu wa Rais amesisitiza kuendelezwa kwa jitihada za matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Japan, na kutafuta fursa zinazohusiana na lugha hiyo, ikiwemo walimu na wakalimani.


Makamu wa Rais amempongeza Balozi Mutatembwa kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Japan, akimtaka ajikite katika nyenzo kuu za kitaifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya CCM, na takwimu rasmi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.


Kwa upande wake, Balozi mteule Mheshimiwa Anderson Mutatembwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua kuiwakilisha Taifa nchini Japan, na kuahidi kuimarisha zaidi ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Japan sambamba na kulinda maslahi ya Taifa.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.