MGOMBEA UBUNGE KILOSA (ACT WAZALENDO) AJA NA MWAROBAINI WA KUMALIZA MIGOGORO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI.
Mgombea Ubunge wa Kilosa kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Hassan Thabiti Mbaruku, amewapa wananchi wa jimbo hilo matumaini mapya baada ya kutoa mwarobaini wa namna atakavyokabiliana na migogoro ya wakulima na wafugaji, changamoto inayokwamisha maendeleo ya kilimo na ufugaji katika eneo hilo.
Ahadi hiyo alitoa Septemba 22, 2025, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu ya ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam, baada ya kukabidhiwa Ilani ya Chama kwa mwaka 2025/2026 kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.
Mgombea huyo kijana, anayejivunia matamanio ya kuleta mageuzi na maendeleo makubwa katika Kilosa, alisema migogoro ya ardhi na malisho ni changamoto sugu inayokwamisha wananchi.
“Migogoro hii imekuwa ikichangia wakulima kutoendelea na wafugaji kupata malisho ya kutosha. Endapo nitachaguliwa, nitahakikisha maeneo maalum yanatengwa kwa kila upande ili shughuli zao ziwe huru na kwa usawa,” alisema Mbaruku.
Aidha, Mbaruku ameeleza kuwa atashirikiana na Serikali katika kupanga maeneo maalum ya kilimo na malisho, pamoja na kuhakikisha eneo la nyasi kwa ajili ya mifugo limetengwa ipasavyo. Anadai kuwa njia hii italeta suluhisho la kudumu kwa migogoro hiyo.
Mbali na hilo, mgombea huyo amejipanga kushughulikia changamoto nyingine muhimu jimboni Kilosa ambapo Pamoja na kuboresha sekta ya afya kwa kuhakikisha Zahanati za Kata zinapandishwa hadhi ya kuwa Vituo vya Afya na kuboresha Hospitali ya Wilaya, atahakikisha pia ajira kwa vijana zinapatikana kupitia kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo vitakavyozalisha ajira na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.
Mbaruku amesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara za mitaa na mifereji ya maji, huku akiahidi pia kufanya maboresho katika sekta ya elimu kwa kuondoa michango isiyo na tija na kuhakikisha shule za msingi na sekondari zinapata rasilimali zinazohitajika.
Mgombea huyo amehimiza wananchi wa Kilosa kupigia kura kuwa mbunge wao sanjari na kushirikiana naye katika jitihada za kuleta amani na maendeleo, akisema kuwa utekelezaji wa mwarobaini huu utagusa kila kona ya jimbo hilo na kuboresha maisha ya wakazi wake kwa ujumla.


Comments
Post a Comment