Mpango Azungumza na Mfuko wa Hasara na Maafa, Akisisitiza Changamoto za Nchi za Afrika.
Na Mwandishi Wetu, New York
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Hasara na Maafa yatokanayo na Mabadiliko ya Tabianchi (Loss and Damage Fund), Ibrahima Diong, pembezoni mwa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kinachoendelea jijini New York, Marekani.
Mazungumzo hayo yalilenga kujadili changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mataifa ya Afrika, ikiwemo Tanzania, pamoja na mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa fedha ili kusaidia nchi zinazoendelea ambazo zinaendelea kuchukua hatua za kukabiliana na madhara hayo licha ya changamoto ya rasilimali fedha.
Mfuko wa Hasara na Maafa kutokana na mabadiliko ya tabianchi (Loss and Damage Fund) uliundwa mahsusi kutoa msaada wa kifedha kwa nchi maskini na zinazoendelea ambazo zinakumbwa na athari za majanga kama mafuriko, ukame na kupanda kwa kina cha bahari, ambazo mara nyingi haziwezi kuzuiwa hata kwa hatua za kukabiliana na tabianchi.
Miongoni mwa malengo ya mfuko huo ni kusaidia nchi zilizo hatarini zaidi, kama visiwa vidogo na nchi zenye kipato cha chini, ambazo kwa kiwango kikubwa zimeathirika na mabadiliko ya tabianchi ingawa zinachangia kidogo katika uzalishaji wa gesi chafu duniani.
Aidha, mfuko huo una lengo la kufidia hasara zisizoepukika, kusaidia ujenzi wa upya wa miundombinu iliyoharibiwa, kuhamisha jamii zilizo katika hatari kubwa na kurejesha maeneo ya kilimo na pwani yaliyoathirika.
Mfuko huo ulianzishwa rasmi katika Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) mwaka 2022 nchini Misri, na katika mkutano wa COP28 mjini Dubai, nchi wanachama zilikubaliana kuanza utekelezaji wake rasmi.




Comments
Post a Comment