NIDA Yawahamasisha Wananchi Kujisajili, Yawahudumia Wenye Ulemavu


Dar es Salaam

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imewataka wananchi kuhakikisha wanajisajili na kupata vitambulisho mara tu wanapofikisha umri wa miaka 18, ili kuepuka msongamano na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu nchini.


Wito huo umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji Vitambulisho NIDA, Edson Guyai, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Utambulisho Duniani.


“Ukifika miaka 18 nenda ukajisajili mara moja. Kitambulisho hiki ndicho kitakachokutambulisha na kukuwezesha kupata huduma zote muhimu,” alisema Guyai.


Katika maadhimisho hayo, NIDA iliwahudumia pia watu wenye ulemavu, hatua iliyopokelewa kwa furaha na viongozi wa ustawi wa jamii pamoja na walemavu wenyewe.


Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Temeke, Restita Bujiku, alisema zoezi hilo limekuwa msaada mkubwa kwao.


“Hii ni fursa muhimu kwa walemavu ambao mara nyingi hawajitokezi kwa wingi kujisajili. Tunashukuru NIDA kwa kutufikia,” alisema Bujiku.


Miongoni mwa walemavu waliosajiliwa, Mabadi Mlawa, alisema vitambulisho hivyo vitawaondoa kwenye utegemezi wa kutumia nyaraka za ndugu na jamaa.


“Mimi naomba wenzangu tuitumie fursa hii. Kitambulisho chetu kitatusaidia kupata huduma bila kikwazo,” alisema.


Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kitambulisho changu, mwavuli wangu”, ikisisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kujisajili na kutambulika rasmi.






Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.