Polisi Mbeya Wakamata Mtuhumiwa wa Mauaji ya Mtoto, Waendelea Kuchunguza Kifo cha Mwanachuo.
Mbeya
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mwanamke mmoja kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa miaka 15 huku pia likiendelea na uchunguzi wa mauaji ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Mzumbe ndaki ya Mbeya.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, tukio la kwanza lilitokea Septemba 16, 2025 katika eneo la DDC Mbalizi, Kata ya Utengule Usongwe, ambapo mwili wa Rehema Sikalengo [15] ulikutwa jikoni nyumbani kwao ukiwa umetumbukizwa kwenye jaba lililokuwa na maji.
SACP Kuzaga amesema mtuhumiwa anayeshikiliwa ni Magreth Jonas Lyanda, mkazi wa Mbozi, aliyekamatwa Septemba 18, 2025 katika eneo la Mlowo, Wilaya ya Mbozi. Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa mtuhumiwa alidaiwa kuhusiana na madai ya ujira wake wa zamani alipokuwa akifanya kazi kwa mama mzazi wa marehemu.
Katika tukio la pili, SACP Kuzaga amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kifo cha mwanafunzi wa sheria, Shairose Michael Mabula [21], aliyeripotiwa kupotea Septemba 14, 2025 na baba yake Dkt. Michael Mabula.
Septemba 16, 2025 kulitokea ajali ya moto katika Mtaa wa Morovian, Kata ya Isyesye Jijini Mbeya ambapo mwili wa binti mmoja ulipatikana baada ya moto kuzimwa. Baada ya uchunguzi wa kitabibu, ilibainika kuwa mwili huo ni wa Shairose Mabula.
SACP Kuzaga amesema uchunguzi wa kina unaendelea, ikiwemo kutumia mbinu za kisayansi kubaini mazingira ya tukio na kuwakamata waliohusika. Aidha, amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kukamatwa kwa wahusika na kuepusha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

Comments
Post a Comment