Serikali Kupitia Wizara ya Mawasiliano Yajipanga Kupanua na kuboresha Mawasiliano Vijijini.
Na Fidea Masunga,Dar es Salaam.
Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, awe mjini au kijijini, anapata huduma bora na za uhakika za simu pamoja na usikivu mzuri wa redio.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Salome Kessy, alisema hayo alipofungua mafunzo ya ndani kwa wataalamu wa Mradi wa Miundombinu ya Mawasiliano Vijijini yanayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 29 hadi Novemba 7, 2025.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kiufundi katika usimamizi wa mitandao ya simu vijijini, uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano, pamoja na utatuzi wa changamoto zinazohusu huduma za simu na intaneti.
Kwa mujibu wa Kessy, kufikia Juni 2025 Tanzania ilikuwa na zaidi ya laini za simu milioni 92, sawa na upenyo wa asilimia 136. Aidha, kulikuwa na watumiaji wa intaneti milioni 54, sawa na upenyo wa asilimia 79.
Alisema huduma za intaneti ya kasi zimewafikia wananchi kwa kiwango cha asilimia 98 kupitia 2G, 93 kwa 3G, 92 kwa 4G na 26 kwa 5G. Hata hivyo, alibainisha kuwa bado matumizi ya simu janja yako chini, yakiwa na upenyo wa asilimia 37 pekee.
“Serikali itaendelea kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ili kuhakikisha kila eneo, hususan vijijini, linafikiwa na huduma za mtandao wa kasi,” alisema Kessy na kuongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA na Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali 2024–2034, kwa lengo la kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano, Mulembwa Munaku, alisema mradi huo unahusisha ujenzi wa minara 636 kati yake, 621 ni ya mawasiliano ya simu na 15 ni ya redio.
Alisema Oktoba 23, 2023 Serikali ilisaini mkataba na kampuni ya China National Technical Import and Export Corporation (CNTIC) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa muda wa miezi 24 kuanzia Desemba 9, 2024 hadi Desemba 8, 2026, kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 108.5 (takriban Sh280 bilioni), fedha zilizopatikana kupitia mkopo nafuu kutoka Benki ya Exim ya China.





Comments
Post a Comment