Tanzania Yalenga Kuwa Kinara wa Uchumi wa Buluu


Dar es Salaam. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuimarisha uchumi wa buluu, ikilenga kuifanya nchi kuwa kinara wa sekta hiyo barani Afrika.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi, wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Wadau wa Uchumi wa Buluu linaloendelea jijini Dar es Salaam ambalo limeandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) pamoja na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar.


Mitawi amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha sekta hiyo kwa kuwa ni eneo lenye fursa kubwa za ajira, biashara na ukuaji wa pato la taifa.


Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya nchi jirani na taasisi za kimataifa ni muhimu kwani bahari haina mipaka hivyo mafanikio katika sekta hiyo yanahitaji mshikamano wa kitaifa, kikanda na kimataifa.


Aidha, amesisitiza kuwa uchumi wa buluu ni eneo lenye fursa kubwa ambazo hazijatumika na zikitumika ipasavyo zitakuwa ni uti wa mgongo wa mageuzi ya maendeleo ya taifa kutokana na kuwepo kwa maeneo makubwa ya vyanzo vya maji.


"Sote tunatambua kuwa uchumi wa buluu unapatikana kupitia mito, bahari, maziwa, misitu na ardhi oevu nchini ambayo yakitumika ipasavyo yataongeza ajira, kukuza biashara, kuimarisha usalama wa chakula hivyo kuboresha maisha ya wananchi," amesema. Bw. Mitawi.


Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchukuzi Bw. Shomari Shomari ameelezea nafasi kubwa ya sekta ya usafirishaji na maboresho ya miundombinu ya bandari katika kuimarisha uchumi wa buluu.

Amebainisha kuwa miradi mikubwa ya kisasa ya reli, maboresho ya bandari na udhibiti wa usafiri na usalama wa majini ni nyenzo muhimu katika kufungua fursa za uchumi wa buluu ikiwemo kukuza biashara na ajira kwa Watanzania


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Profesa Tumaini Gurumo, amesema kongamano hilo lina lengo la kujadili changamoto zinazokabili sekta hiyo na kupata suluhu za pamoja.

“Kongamano hili ni jukwaa muhimu la kitaifa na kimataifa kwa wadau kubadilishana mawazo na mbinu zitakazosaidia nchi yetu kunufaika zaidi na rasilimali za bahari,” amesema Prof. Gurumo.


Kongamano hilo linafanyika katika Ukumbi wa Kingjada Morocco Square, likiwa na kauli mbiu: “Bahari Yetu, Fursa Yetu, Wajibu Wetu”, na litadumu kwa siku mbili kuanzia Septemba 10 hadi 11, 2025.







Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.