TAMWA Yapongeza Wanawake Wagombea Uongozi Katika Uchaguzi Mkuu 2025
Dar es Salaam,
Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimewapongeza wanawake wote waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dkt. Rose Reuben, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA,imesema mchakato wa uteuzi na uchukuaji fomu umeonyesha ari na mwamko mkubwa wa wanawake kushiriki kwenye nafasi mbalimbali za uongozi nchini.
Kulingana na takwimu za Ulingo Wanawake, wanawake 231 walichukua fomu za ubunge kupitia CCM, na kati yao 25 waliteuliwa na chama, wakiwemo nane wapya huku vyama mbalimbali vya siasa vimeongeza idadi ya wanawake wagombea wenza katika nafasi ya urais na makamu wa Rais.
“Kwa namna ya kipekee, TAMWA inampa pongezi za pekee Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliyeteuliwa na CCM kuwa mgombea wa kwanza mwanamke wa urais katika historia ya chama tawala. Hii ni hatua ya kihistoria inayohamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi wa juu nchini.”
TAMWA pia imewatambua wanawake wengine walioteuliwa kugombea urais pamoja na wagombea wenza, wakiwemo:
- Mwajuma Noty Mirambo (UMD) na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji
- Eveline Wilbard Munis (NCCR)
- Husna Mohamed Abdallah (CUF)
- Aziza Haji Selemani (MAKINI)
- Amani Selemani Mzee (TLP)
- Chausiku Khatibu Mohamed (NLD)
- Sakia Mussa Debwa (SAU)
- Chuma Juma Abdallah na Devotha Minja (CHAUMA)
“TAMWA inathamini ujasiri na kujituma kwa wanawake wote waliojitokeza au kujaribu kugombea, licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili. Chama kimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi kupitia warsha, makongamano, mijadala, na vyombo vya habari ili kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanawake.”
Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha kuwa hadi Februari 2024, wanawake walikuwa asilimia 37.4 ya wabunge (148 kati ya 392), wengi wao wakiwa kupitia viti maalum. Ripoti za Aprili na Julai 2024 zinaonyesha asilimia 37.5 ya mawaziri ni wanawake.
TAMWA imesisitiza kuwa uwepo wa wanawake katika nafasi za uongozi ni muhimu kwa maendeleo ya taifa, kwani unachangia usawa wa kijinsia, uwajibikaji, na kulinda maslahi ya makundi yote, hususan wanawake na watoto. Chama kinasisitiza uwajibikaji wa jamii, vyama vya siasa, serikali, na wadau kuhakikisha wanawake wanapata nafasi sawa katika siasa na uongozi.
Aidha, TAMWA imetoa wito wa kampeni safi, jumuishi na zenye staha, zinazolenga ustawi na utu wa jamii, badala ya matusi, kejeli au ubaguzi wa kijinsia. Chama kinasisitiza kufuatilia kampeni zote na kuripoti wagombea wanaokiuka kanuni za uchaguzi.

Comments
Post a Comment