TUME YA UCHAGUZI YAMTEUA DK. KHALID SALUM KUWA MWAKILISHI WA JIMBO LA DONGE.


Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imemteua na kumtangaza rasmi Dk. Khalid Salum Mohamed wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo la Donge kwa kipindi cha mwaka 2025–2030.


Uteuzi huo umefanyika baada ya Dk. Khalid kuteuliwa na tume hiyo kuwa mgombea pekee, kufuatia mgombea wa chama cha ACT Wazalendo kushindwa kukidhi vigezo vya uteuzi.


Akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Mahonda, Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ya Wilaya ya Kaskazini B, Mwanamkuu Gharibu Mgeni, alisema uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 59(a) na (b) cha Sheria ya Uchaguzi namba 4 ya mwaka 2018.


Aidha, Msimamizi huyo alieleza kuwa tume imefanya uteuzi wa wagombea wa udiwani katika wadi za Mkataleni, Vijibweni na Kiwengwa, Wilaya ya Kaskazini B.


Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mashauri Shehe Khamis (CCM) ameteuliwa na kutangazwa kuwa Diwani wa Wadi ya Vijibweni baada ya kuwa mgombea pekee, huku Omar Haruna Abu (CCM) akiteuliwa kuwa Diwani wa Wadi ya Mkataleni. Pia, Mtumwa Juma Mshamba ametangazwa kuwa Diwani wa Wadi ya Kiwengwa kupitia chama hicho hicho.


Mara baada ya kutangazwa, Dk. Khalid aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Donge kuwatumikia bila kujali tofauti za kisiasa, dini wala rangi, akisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wote.


“Nitahakikisha Jimbo la Donge tunashinda kwa kishindo, kuanzia kura za urais wa Zanzibar, urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na mbunge wetu wa jimbo la Donge,” alisema Dk. Khalid.


Kwa upande wake, Diwani mteule wa Wadi ya Kiwengwa, Mashauri Shehe Khamis, alisema atashirikiana na wagombea wengine wa chama hicho jimboni humo kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.