Wataalamu wa Uchukuzi Watakiwa Kusaka Fursa za Uchumi wa Buluu.
Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, amewaagiza wataalamu wa sekta ya uchukuzi pamoja na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kujikita katika tafiti za kina zitakazochochea uwekezaji kupitia sekta ya uchumi wa buluu, akisisitiza kuwa hatua hiyo ndiyo njia ya kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Prof. Kahyarara alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga kongamano la kitaifa la uchumi wa buluu lililoandaliwa na DMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Alisema rasilimali za bahari, mito na maziwa ambazo Tanzania imejaaliwa ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa, na zinapaswa kutumiwa ipasavyo katika kuongeza pato la taifa na kuimarisha uchumi.
“Tunapaswa kutumia fursa tulizonazo kwa utafiti na ubunifu ili kuchambua maeneo muhimu ya uwekezaji yatakayoongeza tija. Hii ndiyo njia ya kuhakikisha uchumi wetu unakuwa shindani na endelevu,” alisema Prof. Kahyarara.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Prof. Tumaini Gurumo, alisema kongamano hilo limeibua maazimio kadhaa, ikiwemo kuandaa mpango wa utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu unaozingatia uhimilivu wa mazingira kwa maendeleo endelevu.
Alibainisha kuwa ni muhimu elimu ya uchumi wa buluu ianze kutolewa kuanzia ngazi za awali ili kujenga uelewa wa mapema miongoni mwa watoto, kwa kuwa taifa limeamua sekta hiyo kuwa miongoni mwa injini kuu za kukuza pato la taifa.
“Tunapaswa kuhakikisha vijana na wanawake wanashirikishwa kikamilifu katika sekta zote za uchumi wa buluu, sambamba na kuongeza uwekezaji wa makusudi katika tafiti na bunifu zitakazochochea ukuaji wa sekta hii. Hii ndiyo njia ya kutengeneza taifa tunalolitaka lenye uchumi wa buluu endelevu,” alisisitiza Prof. Gurumo.
Aidha, aliongeza kuwa usalama na ulinzi wa maeneo ya maji lazima upewe kipaumbele ili kulinda rasilimali na kuhakikisha shughuli zote za kiuchumi zinafanyika kwa uendelevu.
Kongamano hilo la siku mbili lililoanza Septemba 10 na kufungwa Septemba 11, 2025, liliwakutanisha wadau mbalimbali wa uchumi wa buluu kutoka taasisi za serikali na binafsi huku kongamano hilo likiwa limebebwa na kaulimbiu isemayo: “Bahari Yetu, Fursa Yetu, Wajibu Wetu.”



Comments
Post a Comment