ASASI ZA WANAWAKE ZAHIMIZA USHIRIKI WA WANAWAKE KWENYE UCHAGUZI, ZAKEMEA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA.
Na Fidea Masunga, Dar es Salaam
MUUNGANO wa asasi za wanawake na watetezi wa usawa wa kijinsia umetoa wito kwa wanawake nchini kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi, sambamba na kulaani vitendo vya udhalilishaji vinavyowakandamiza wanawake wanasiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa jijini Dar es Salaam, Muasisi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Haji Mwalimu, alisema ushiriki wa wanawake katika siasa ni nguzo muhimu ya kukuza demokrasia jumuishi na kuhakikisha masuala yanayowagusa wanawake, watoto na vijana yanapewa kipaumbele.
Alisema mwaka huu Tanzania imepiga hatua kubwa katika ajenda ya usawa wa kijinsia kisiasa, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan anawania tena urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wanawake wengine wawili Saumu Rashid (UDP) na Mwajuma Mirambo (UMD) wakigombea nafasi hiyo.
Aidha, idadi ya wagombea wenza wanawake imeongezeka katika vyama mbalimbali vikiwemo NCCR, CUF, DP, TLP, NLD, SAU na CHAUMA.
“Uongozi bora hauna jinsia bali uwezo, maadili na dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi,” alisema Rose, akilaani vikali vitendo vya kejeli, matusi na mashambulizi ya kibinafsi vinavyowalenga wanawake wanasiasa.
Kwa upande wake, Janet John kutoka shirika la Binti Makini, aliwataka wanawake vijana kujiamini na kushiriki siasa bila hofu, akisisitiza kuwa sauti yao ni msingi wa mabadiliko chanya katika jamii.
“Tunahitaji kuona wanawake wakijitokeza si tu kupiga kura, bali pia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia udiwani hadi ubunge,” alisema Janet.
Naye Lucy Kilasi kutoka shirika la Women Welfare Tanzania alisisitiza umuhimu wa kuandaa mazingira salama kwa wanawake katika siasa, akisema ukatili wa kijinsia na lugha za kudhalilisha zinawakatisha tamaa wanawake wengi kushiriki.
“Tunaomba vyombo vya usimamizi wa uchaguzi kuhakikisha haki na usalama wa wanawake zinalindwa kikamilifu,” alisema Lucy.
Asasi hizo pia zimepongeza uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia kupitia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5), inayolenga kuwawezesha wanawake na wasichana.
Asasi zilizotoa tamko hilo ni Ulingo Wanawake, Women Welfare Tanzania (WFT), TAMWA, Binti Makini, WAJIKI, WILDAF, Young and Alive, Generation Act, na TAWIA.




Comments
Post a Comment