BALOZI YAKUB APONGEZA MUHIMBILI KUPELEKA WATOA HUDUMA ZA KIBINGWA WENGI NCHINI COMORO.
Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakub, ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kupeleka idadi kubwa ya madaktari bingwa na bobezi kushiriki katika kambi ya matibabu inayoendelea nchini humo.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa wakati wa ziara yake visiwani Comoro.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Afisa Habari wa MNH, Balozi Yakub alisema hospitali hiyo imepeleka jumla ya madaktari bingwa saba kutoka fani mbalimbali, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na taasisi nyingine zinazoshiriki kambi hiyo.
“Hospitali ya Muhimbili imetuletea zaidi ya madaktari saba. Wataalam hawa watahudumia wagonjwa wa figo, ngozi, macho, meno, masuala ya uzazi kwa akina mama pamoja na magonjwa ya wanawake,” alisema Balozi Yakub.
Aidha, alibainisha kuwa ingawa kambi ya matibabu inatarajiwa kuanza rasmi Oktoba 4, 2025, tayari zaidi ya watu 1,000 wamejisajili kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, jambo linaloonesha mwitikio mkubwa wa wananchi wa Comoro.



Comments
Post a Comment