Matokeo ya CIP-Africa Yaonyesha CCM Inaungwa Mkono Zaidi, Wananchi Wapongeza Tume Huru ya Uchaguzi.
Kituo cha Sera za Kimataifa – Afrika (CIP-Africa) kimetoa matokeo ya kura ya maoni kuhusu mwelekeo wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 29, 2025, yakionesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaendelea kuungwa mkono zaidi na wananchi katika maeneo mengi ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Tafiti na Uchapishaji wa CIP-Africa, Thabiti Mlangi, alisema matokeo hayo yanaonyesha kuwa asilimia 91ya wananchi wameridhishwa na usimamizi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), huku asilimia 83 wakieleza dhamira ya kushiriki kupiga kura siku ya uchaguzi.
Aidha matokeo hayo yanaonyesha CCM ikiongoza katika mikoa kadhaa ikiwemo Dodoma (91.4%), Morogoro (87%), Tanga (95.3%), Tabora (87.6%), na Ruvuma (89%).
Vyama vingine vilipata kati ya 1.5% hadi 10% ya uungwaji mkono, huku asilimia 46 ya wananchi wakisema wanavutiwa na sera za vyama vya siasa.
Mlangi alibainisha masuala muhimu ambayo wananchi wanataka serikali ijayo iyape kipaumbele ni pamoja na Upatikanaji wa maji safi (78%),Elimu bora (78%),Barabara na madaraja (69%),Huduma bora za afya (63%),Mapambano dhidi ya rushwa (60%) na Uimarishaji wa demokrasia (47%).
Aidha, baadhi ya wananchi wameeleza wasiwasi juu ya kuongezeka kwa matumizi ya bhangi miongoni mwa wanafunzi,huku wakitaka hatua madhubuti zichukuliwe kudhibiti tatizo hilo.
Akizungumza kuhusu wito kwa wananchi kuhusu uchaguzi wa October 29 Mlangi alisema:
“Tunawasihi Watanzania wajitokeze kwa wingi tarehe 29 Oktoba, kupiga kura kwa amani na utulivu. Kumbukeni kuna maisha baada ya uchaguzi,” alisema Mlangi.
Kura hiyo ya maoni ilifanyika kati ya Septemba 30 na Oktoba 5, 2025 katika mikoa 19, ikihusisha wananchi 1,976.

Comments
Post a Comment