Dkt. Samia kutua Temeke kwa ajili ya kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu
Na Fidea Masunga,Dar es salaam.
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwasili katika Wilaya ya Temeke tarehe 23 Oktoba 2025 kwa ajili ya kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Temeke, Zena Yussuf Mgaya, amesema maandalizi ya mapokezi ya mgombea huyo yamekamilika, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumsikiliza.
“Tunawaomba wananchi wa Temeke wajitokeze kwa wingi kumsikiliza Dkt. Samia. Ni fursa muhimu ya kufahamu mafanikio yaliyotekelezwa na mwelekeo wa maendeleo kwa awamu ijayo,” amesema Mgaya.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Wilaya ya Temeke, Daniel Sayi, amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi kuelekea uchaguzi huo, akisisitiza kupuuza watu wenye nia ovu ya kuchochea vurugu.
“Kwa kipindi hiki cha kampeni kumekuwa na watu wachache wenye lengo la kuchafua amani. Tunawaomba wananchi wa Temeke na Watanzania kwa ujumla wawapuuze na wajitokeze kupiga kura kwa amani,” amesema Sayi.
Aidha, Sayi amesema CCM inaendelea kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa Ilani ya chama hicho, ikiwemo katika sekta ya afya, ambapo Hospitali ya Temeke imepandishwa hadhi kuwa hospitali ya rufaa, hatua iliyoboresha kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wa eneo hilo.
“Kupandishwa hadhi kwa Hospitali ya Temeke ni kielelezo cha dhamira ya serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za jamii,” amesisitiza Sayi.





Comments
Post a Comment