EWURA Yatangaza Bei Kikomo za Mafuta Oktoba 2025
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo za mafuta ya petroli zitakazotumika kuanzia Jumatano, Oktoba 1, 2025 saa 6:01 usiku.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Mwainyekule, amesema mabadiliko ya bei yametokana na mwenendo wa soko la dunia, ambapo bei za mafuta yaliyosafishwa zimeongezeka kwa asilimia 2.80 kwa petroli, asilimia 3.65 kwa dizeli, na asilimia 3.57 kwa mafuta ya taa. Gharama za kubadilisha fedha za kigeni zimepungua kwa wastani wa asilimia 5.10%.
“Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maagizo haya,” amesema Dkt. James Mwainyekule, akisisitiza kulinda maslahi ya wananchi na kuhakikisha ushindani wa kibiashara unaendelea.
Wananchi wanashauriwa kutumia huduma ya bure ya kukagua bei kikomo kupitia simu za mkononi kwa kupiga namba 15200#, huduma inayopatikana kwa mitandao yote ya simu nchini. Hii itawawezesha wananchi kuthibitisha bei za mafuta katika eneo lao kabla ya kununua.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa zao kwa bei ya ushindani, mradi zisizozidi bei kikomo au kuwa chini ya bei ya chini iliyoruhusiwa. EWURA itaendelea kutoa taarifa za bei kikomo kila mwezi ili kuhakikisha uwazi wa soko, ushindani, na ulinzi wa maslahi ya mlaji.
Kwa mwezi Oktoba 2025, mabadiliko haya yanatarajiwa kuathiri bei ndogo za rejareja na jumla katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, huku EWURA ikisisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la mafuta duniani na kutoa taarifa kwa umma kila mwezi.




Comments
Post a Comment