HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA NA INTERBURNS YA UINGEREZA WAKUBALIANA KUBORESHA HUDUMA ZA MATIBABU YA MAJERAHA YA MOTO.
Dodoma.
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa kushirikiana na Interburns Society ya Uingereza zimesaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye majeraha ya moto, ikiwemo kuanzisha kitengo na wodi maalumu kwa ajili ya huduma hizo.
Hati hiyo imesainiwa jijini Dodoma, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, kama sehemu ya mpango wa kuimarisha utoaji wa huduma za kibingwa na kuongeza uwezo wa kitaalamu katika matibabu ya majeraha makubwa ya moto nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, alisema makubaliano hayo yatachangia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha huduma kwa wagonjwa na kukuza ujuzi wa wataalamu wa afya.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Interburns Society, Bi. Tina Bajec, alieleza kuwa taasisi yake imejipanga kushirikiana na Tanzania katika kuboresha huduma za afya, hususan kwa wagonjwa walioungua moto.
Naye, Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Moto hospitalini hapo, Dkt. Samwel Wambura, alisema ushirikiano huo utakuwa chachu ya kuimarisha huduma za wagonjwa wa moto nchini.
Hafla hiyo imekuja wakati Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiadhimisha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, ikiwa inaendelea kupanua wigo wa ushirikiano wa kitaifa na kimataifa katika kuboresha huduma za afya nchini.




Comments
Post a Comment