Madaktari Bingwa Amana Warejesha Tabasamu kwa Mwanamke Aliyeteseka na Uvimbe wa Kilo 12 Tumboni.
Dar es Salaam.
Madaktari bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana wamefanikiwa kumfanyia upasuaji wa kuondoa uvimbe mkubwa wenye uzito wa kilo 12 kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 60, hatua iliyorejesha matumaini na tabasamu kwake baada ya muda mrefu wa kuishi na maumivu makali.
Akizungumza mara baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi wa hospitali hiyo, Dkt. Getrude Kimario, amesema mgonjwa huyo alifika hospitalini akilalamika kwa muda mrefu kuhusu maumivu tumboni na kuvimba sehemu ya chini ya tumbo. Baada ya kufanyiwa vipimo vya kina, waligundua kuwa alikuwa na uvimbe mkubwa kwenye kiwanda cha mayai ya uzazi upande wa kushoto.
“Hii ni mara ya kwanza kukutana na mgonjwa mwenye uvimbe mkubwa kiasi hiki, lakini tunamshukuru Mungu tumefanikisha kuutoa. Upasuaji umeenda vizuri na mgonjwa anaendelea kuimarika,” alisema Dkt. Kimario.
Kwa mujibu wa maelezo yake, uvimbe huo ulikuwa umechukua nafasi kubwa tumboni mwa mgonjwa na kumfanya ashindwe kufanya shughuli zake za kawaida kwa muda mrefu.
Baada ya upasuaji, uvimbe huo umehifadhiwa na utapelekwa maabara kwa uchunguzi zaidi ili kubaini aina yake na hatua zinazoweza kuchukuliwa kitabibu.
Aidha, Dkt. Kimario alibainisha kuwa mafanikio ya upasuaji huo yametokana na mshikamano wa timu ya madaktari bingwa na wauguzi wa hospitali ya Amana, waliokuwa na uzoefu wa kutosha katika kushughulikia magonjwa ya akinamama na upasuaji wa aina mbalimbali.
Dkt. Kimario ametoa wito kwa wananchi, hasa wanawake, kujenga mazoea ya kufanyiwa uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kubaini matatizo ya kiafya mapema kabla hayajafikia hatua kubwa inayoweza kuhatarisha maisha.



Comments
Post a Comment