MAKARANI WAONGOZAJI WAPIGAKURA WAFUNDWA NA MSIMAMIZI WA UCHAGUZI JIMBO LA MAFINGA MJINI.


Mafinga Mjini – Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Mafinga Mjini, Bi. Dorothy Kobelo, amefungua mafunzo ya makarani waongozaji wapiga kura akisisitiza kuwa dhamana ya kusimamia uchaguzi ni kubwa, nyeti na muhimu kwa mustakabali wa taifa.


“Dhamana mliyopewa ya kusimamia uchaguzi ni kubwa na nyeti. Mmeteuliwa kwa mujibu wa sheria, kwa kufuata katiba, na mpo hapa kwa niaba ya Tume Huru ya Uchaguzi katika vituo 209 mtakavyopangiwa katika Kata 9,” alisema Bi. Kobelo wakati akizungumza na makarani hao kwenye Ukumbi wa Shule ya Sekondari Changarawe, Halmashauri ya Mji Mafinga.


Alisema kuwa makarani wanapaswa kuhakikisha hawakuwa chanzo cha malalamiko kwa vyama vya siasa, kutumia lugha nzuri wanapotoa huduma, na kutoa kipaumbele kwa watu wenye mahitaji maalum siku ya kupiga kura.


Aidha, makarani hao walikula kiapo cha kutunza siri, kiapo kilichoongozwa na Wakili Msomi, Mwanasheria wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Gaspar Kalinga. Kiapo hicho kinahakikisha kuwa makarani wanatunza siri ya wapiga kura na kutoa huduma kwa uadilifu.


Naye Afisa Uchaguzi, Ndugu Benedict Kibiki, alisema kuwa mafunzo ya makarani 209 yanafanyika siku moja, huku mafunzo ya wasimamizi na wasaidizi wao yakiwa na muda wa siku mbili.


Kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Uchaguzi, uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani utafanyika Tarehe 29 Oktoba 2025, siku ya Jumatano. Jimbo la Mafinga Mjini ni mojawapo ya majimbo 272 nchini Tanzania yatakayoshiriki uchaguzi huo.


Bi. Kobelo na Afisa Uchaguzi Kibiki walisisitiza umuhimu wa kila raia kushiriki katika uchaguzi kwa kusema:


“KURA YAKO, HAKI YAKO – JITOKEZE KUPIGA KURA!”



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.