Mhe. Doyo Kuondoa Mfumo wa Kikokotoo; Aahidi Vivuko Vipya Vinne Kigamboni.


Kigamboni, Dar es Salaam.


Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Doyo, amesisitiza katika mkutano wake wa kampeni wilayani Kigamboni kuwa mfumo wa sasa unaotumika kuwapangia wastaafu na watumishi wa umma matumizi ya fedha zao baada ya kustaafu ni dharau na unaowafanyia wastaafu uonevu.


Akizungumza mbele ya wananchi wa Kigamboni, Mhe. Doyo amesema kuwa serikali ya sasa imeweka utaratibu wa kikokotoo kwenye fedha za wastaafu zilizokusanywa kwa ajili ya akiba ya baada ya kustaafu, kisha inawapangia matumizi kwa awamu kupitia mfumo wa mahesabu. Amesema hali hii ni kinyume na heshima inayostahili kwa wastaafu ambao wamejitolea kwa muda mrefu katika huduma za umma.



“Wastaafu hawana sababu ya kupangiwa matumizi ya fedha zao. Baada ya kustaafu, mtu anatakiwa kupewa fedha zake moja kwa moja ili aweze kuanza maisha mapya kwa uhuru, kuwekeza au kutimiza malengo yake binafsi,” amesema Mhe. Doyo.



Mhe. Doyo ametoa ahadi kwa wananchi kwamba iwapo watamchagua kuwa Rais, mfumo huu wa kupanga matumizi kwa wastaafu utaondolewa. Amesema kila mstaafu atapewa fedha zake kwa ukamilifu, akiwa na uhuru wa kuamua jinsi anavyotaka kuzitumia. Hii, amesema, itawawezesha wastaafu kupanga maisha yao, kuwekeza katika biashara au kilimo, na kuchangia maendeleo ya jamii zao na taifa kwa ujumla.


Aidha, Mhe. Doyo amesisitiza umuhimu wa kuwaandaa watumishi wa umma waliokaribia kustaafu kupitia elimu ya kifedha. Amefafanua kuwa mpango huu utahusisha mafunzo ya kupanga bajeti binafsi, fursa za uwekezaji salama na zinazozalisha faida, ushauri wa kifedha, na mbinu za kuepuka matumizi yasiyo na tija. Lengo, amesema, ni kuhakikisha kila mstaafu anatumia fedha zake kwa hekima, bila kulazimishwa na vizuizi vya serikali, na kufanikisha ustawi wake pamoja na wa familia yake.


Faida za mfumo huu mpya ni nyingi, ikiwemo kuwapatia wastaafu uhuru wa kifedha, kuongeza uwekezaji katika shughuli za kimaendeleo, na kukuza ustawi wa familia zao. Vilevile, kuondolewa kwa mpangilio wa mahesabu ya serikali kutapunguza urasimu, na kuhakikisha kila mstaafu anapata kile alichokusanya kwa heshima.

 

“Baada ya kustaafu, mtu anatakiwa kuanza maisha mapya kwa heshima na uhuru wa kifedha. Serikali yangu itahakikisha kila mstaafu anapata kile alichokusanya, akiwa na maarifa ya kutumia fedha hizo kwa maslahi yake binafsi na jamii.” amesema Mhe. Doyo


Kwa mujibu wa Mhe. Doyo, mfumo huu mpya unalenga kutoa heshima, uhuru na fursa kwa watumishi waliotumikia taifa kwa miongo kadhaa, huku ukichangia maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi wote.


Pia akizungumza swala la Kivuko cha Kigamboni, Mhe. Doyo ameongeza kuwa serikali yake itaimarisha huduma za usafiri wa majini ili kuboresha maisha ya wananchi wa Kigamboni na maeneo jirani. Amesema huduma za vivuko vya sasa hazikidhi mahitaji ya wananchi kutokana na uchache wa vyombo na muda mrefu wa kungojea kuvuka, hali inayochelewesha shughuli za kiuchumi na kijamii.


“Tutakapounda serikali ya NLD, tutanunua vivuko vipya vinne vitakavyotoa huduma endelevu kwa wakazi wa Kigamboni. Tunataka wananchi waweze kuvuka kwa haraka bila foleni ndefu, ili wachangie ipasavyo katika pato la taifa,” amesema Mhe. Doyo.


Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Kina Mama Taifa, Bi. Zaidat Fundi Majiamoto, amesema kuwa mfumo wa sasa wa kikokotoo kwa wastaafu umekuwa ukiwathiri kina mama wengi ambao walikuwa nguzo kuu katika familia na utumishi wa umma. Amesema iwapo mfumo wa malipo ungekuwa mzuri na wa haki, wastaafu wengi, hususan kina baba, wangeweza kujitegemea baada ya kustaafu, hivyo kupunguza mzigo unaowaangukia kina mama.


“Kina mama wengi wamelazimika kuingia kwenye mikopo kandamizi isiyo na tija ili kuwasaidia waume zao waliostaafu ambao hawakupata mafao yao kwa wakati au kwa ukamilifu. Tumchagueni Doyo ili wastaafu wapate mfumo mpya, na kina mama tupate afueni ya kuondokana na mikopo hii isiyo na tija,” amesema Bi. Majiamoto.



Tayari Chama cha NLD kimefika zaidi ya mikoa 27 katika kampeni zake, na viongozi wa chama hicho wanatarajiwa kuelekea Zanzibar na Tanga kuendelea na mikutano ya kampeni.

Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.